Na Innocent Mungy
DAR ES SALAAM, Septemba 25, 2023 – Katika hatua muhimu kwa Sekta ya Mawasiliano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano ya maridhiano na watoa huduma wa mawasiliano yenye thamani ya Shilingi bilioni 50 kama malipo ya matumizi ya miundombinu tangu kujengwa kwake. Aidha, Watoa Huduma hao wameahidi pia uwekeza Shilingi bilioni 32.5 katika maendeleo ya miundombinu zaidi nchini.
Serikali ya Tanzania imefikia makubaliano haya ya kihistoria na watoa huduma wa mawasiliano nchini katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Dar es Salaam leo tarehe 25 Septemba 2023 katika Hoteli ya Serena. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Vingozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu na watoa huduma wa mawasiliano nchini. Makubaliano haya yanalenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, na yalijumuisha kampuni kubwa za simu za Airtel Tanzania, Honora Tanzania (Tigo), na Vodacom Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi wa Tanzania.
Waziri Nnauye alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujitolea kwake kukuza Sekta ya Mawasiliano. Mheshimiwa Nape pia alielezea dhamira ya serikali kuhakikisha huduma za Mawasiliano zinawafikia wananchi wote na kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Aliwapongeza viongozi wa serikali walioshiriki katika majadiliano na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya mawasiliano nchi ili kufikia uchumi wa kidijitali.
Makubaliano haya ya kihistoria yalianzishwa mnamo Oktoba 4, 2011, na yalilenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa mkongo wa taifa katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma ya mawasiliano. Wakati wa hafla ya utiaji saini, watoa huduma wa mawasiliano walikubaliana kutoa dola milioni 20 kwa matumizi ya kipindi cha miaka mitano na kuahidi kuwekeza dola milioni 13 katika maendeleo ya miundombinu zaidi.
Hafla hiyo pia ilishuhudia kujiunga kwa Vodacom Tanzania kama mwanachama wa muungano huo, ikionyesha ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali katika kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi na kukuza uchumi.
Serikali imedhamiria inafikia lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia Watanzania wote na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali, na inalenga kufikia asilimia 85 ya Watanzania wenye ufikiaji wa intaneti ya kasi ifikapo mwaka 2025.
Aidha Waziri Nnauye alitoa maelekezo ya utekelezaji wa makubaliano haya na kuwasihi watoa huduma wa mawasiliano kuendelea kuwekeza katika miundombinu ili kufikia wananchi wengi zaidi. Hafla hii ilipokelewa kwa furaha kutoka pande zote mbili na inaonyesha hatua muhimu kuelekea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini Tanzania.