DKT. NDUMBARO: HAIKUWA KAZI RAHISI KUSHINDA KUANDAA AFCON 2027

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema
haikuwa kazi rahisi kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kushinda zabuni ya
kuandaa Fainali za Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Dkt. Ndumbaro amesema hayo Septemba 29, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa
kwenye mkutano na waandishi wa Habari kuhusu nchi hizo za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuandaa mashindano hayo makubwa barani Afrika.

“Haikuwa kazi ndogo, ilikuwa kazi ngumu sana, tuliweka mikakati ya pamoja ya kutosha
kuhakikisha zabuni yetu ambayo sasa ni EA Pamoja AFCON 2027 inashinda. Mipango
yetu ilikuwa na nguvu na msukumo wa Marais wetu watatu; Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Mhe. Dkt. William Samoye Ruto na Mhe. Jenerali Yoweri Kaguta Museveni
utayari na mchango wao kwenye mashindano haya kwetu ulikuwa mtaji wa kwanza”
amesema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro amesema Wizara itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kujenga viwanja
vipya viwili na kusisitiza maandalizi mengine yafanyike haraka na kwa wakati ili
Watanzania wanufaike.

Vigezo ambavyo vimetumika kushinda zabubi hiyo ni pamoja na Serikali zote tatu ziwe
na dhamana ya Dola za Marekani Milioni 30 kwa kila nchi ambapo jumla yake ni Dola
za Marekani Milioni 90, viwanja sita vya mashindano na kila nchi inapaswa kuwa na
angalau viwanja viwili ambapo kwa Tanzania upo Uwanja wa Benjamin Mkapa umekidhi
sifa na unaendelea kufanyiwa ukarabati wa awamu ya kwanza, Uwanja wa Aman
Zanzibar, huu unaendelea na maboresho huku Uwanja mpya wa Arusha unatarajiwa
kujengwa na kukamilika kabla ya mashindano ya AFCON 2027.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Bw. Wallace Karia
amesema anawashukuru mawaziri wote wa michezo, Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro,
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tanzania, Mhe. Ababu Namwamba, Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Kenya na Mhe. Peter Ogwang, Waziri wa Nchi
Elimu na Michezo, Uganda kwa kazi kubwa waliyoifanya kufanikisha ushindi huo nan
chi hizo kupewa dhamana ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *