MHE. MWINJUMA AFANYA MAZUNGUMZO NA SHULE YA SANAA ESMA UFARANSA

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Shule ya Sanaa ya ESMA iliyopo katika Jiji la Montpellier nchini Ufaransa, imekubali kuanzisha ushirikiano na Taasisi ya Utamaduni na Sanaa Bagamoyo (TaSUBa) kwa lengo la kubadilishana uzoefu na utalaamu utakaokuza na kuendeleza Sekta hiyo katika nchi hizo.

Mhe. Mwinjuma ametoa kauli hiyo mara baada kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shule hiyo Bw. Karim Khenissi leo Oktoba 11, 2023 alipoitembelea, ambayo inatoa elimu ya ufundishaji wa video za michezo , “ video games” na “animation”.

“Tumefanya ziara katika Shule hii, tumeona jinsi wanavyozalisha kazi mbalimbali za Sanaa na kuandaa Wataalamu katika fani hii, tumewakaribisha Tanzania waje wabadilishane uzoefu na Vyuo vyetu vinavyofundisha fani hizo, hususani TaSUBa na wamekubali” amesema Mhe. Mwinjuma.

Mhe. Mwinjuma yupo nchini Ufaransa akiongoza Watanzania katika Maonesho ya Sanaa kati ya Ufaransa na Afrika yanayofanyika Jijini hapo, ambapo Tanzania inashiriki ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano yaliyoingiwa kati ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *