Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa ametoa rai kwa Wasanii wawe mstari wa mbele kuulinda Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa kufanya marejesho ya mikopo kwa wakati ili uweze kuendelea kuhudumia wengine.
Katibu Mkuu Msigwa ameyasema hayo leo Oktoba 13, 2023 alipotembelea Ofisi za Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya Wasanii ambao tayari wamenufaika na mikopo inayotolewa na Mfuko huo.
“Hizi fedha zinategemea mzunguko kwa hiyo unapochukua mkopo hakikisha unarejesha kwa wakati ili wengine wapate na kuufanya hai wakati wote” Amesema Bw. Msigwa.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuinua sekta ya sanaa kwa kuwa ina umuhimu mkubwa sana kwa jamii hasa ikibadilishwa kuwa bidhaa inayoweza kurejesha utimamu wa mwili na akili kupitia burudani.
Amesema sekta ya sanaa inaendana na mabadiliko ya Teknolojia yanayowalazimu wasanii waeendelee kuhitaji huduma ya mikopo, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanaendelea kuthamini juhudi za Serikali kwa kuutunza Mfuko huo.
Kwa upande wao Wasanii walionufaika akiwemo Muhsin Awadhi (Dkt. Cheni) na Abdul Msanga wakizungumza kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuwathamani na kuanzisha mfuko huo ambao umewawezesha kupata mikopo kwa wakati na kufanya shughuli zao kwa ubora na thamani.
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa katik ya pamoja na Muhsin Awadhi (Dkt. Cheni)
picha ya pamoja Katibu mkuu na wadau wa mfuko wa utamaduni