NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KAMISHNA BENEDICT WAKULYAMBA AKAGUA MRADI WA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE

Na: Zainab Ally – Mikumi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamisha Benedict Wakulyamba amesema Miradi ya Ujenzi wa Viwanja vya ndege vinavyoendelea kujengwa katika Hifadhi za Taifa za Mikumi na Ruaha itaenda kuongeza kasi ya ukuwaji katika Sekta ya Utalii hasa katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania.

Kamishna Benedict Wakulyamba amebainisha hayo alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Oktoba 12, 2023 na kukagua ujenzi na Ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kikoboga wenye urefu wa Kilomita 1.8 utakaozingatia taratibu zote za Ujenzi wa Viwanja vya ndege Duniani.

Aidha Wakulyamba amesema Ujenzi wa Kiwanja hicho ni mapinduzi makubwa katika Sekta ya Utalii ikizingatiwa changamoto za miundombinu mbalimbali zimeanza kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuchagiza maendeleo katika Sekta hiyo.

Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi ambaye ni Mratibu wa Mradi wa REGROW Kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Michael Joseph alisema uwanja huo utakuwa na uwezo wa kutua ndege zenye ukubwa wa Q 300 na uwezo wa jengo litakalopokea abiria 140 pamoja na maegesho ya ndege 7.

Awali, wakati akitoa taarifa za Ujenzi wa uwanja huo kwa Naibu Katibu Mkuu, Bw. Michael alisema ujenzi wa mradi huo hauathiri shughuli zozote za utalii katika hifadhi hiyo kwa kutumia uwanja wa zamani, ambapo ndege za kitalii zinaingia kupitia uwanja wa zamani.

Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ignasi Gara alitolea ufafanuzi juu ya kasi kubwa ya kuongezeka kwa idadi ya watalii katika hifadhi hiyo ambapo mafuriko ya Watalii wa ndani wamezidi kuongezeka kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu mbalimbali.

“Kwa mwaka Uliopita tulitazamia kupata watalii elfu 60,000, lakini kwa bahati nzuri baada ya kuanza kwa matengenezo ya uwanja takapata watalii Zaidi 100,000 ambapo tulivuka malengo, Tunaamini hata mwaka huu tutaendelea kupata idadi ya watalii wengi Zaidi” Alisema Kamishna Msaidizi Gara.

Kwaupande Naibu Kamishana wa Uhifadhi na maendeleo ya Biashara Helman Bathiho alisema ukarabati wa Miundombinu ya Barabara pamoja viwanja vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Mikumi, Ruaha pamoja na Nyerere kunatajwa kutoa fursa kwa Watanzania katika kuwekeza katika ujenzi wa Hoteli za Kisasa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla

Aidha Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma rafiki ndani ya hifadhi ikiwemo kuongeza maeneo ya malazi pamoja na kuongeza bidhaa mpya za utalii ili kuchagiza ukuaji katika sekta hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *