WIZARA YA MALIASILI NA UTAMADUNI ZATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA

Na John Mapepele

Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo leo zimekutana kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan ya kuandaa mkakati wa pamoja wa kufungamanisha utalii na utamaduni ili kuongeza pato la taifa.

Katika kikao hicho ambacho kimeongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo, Dkt. Hassan Abbasi (Maliasili na Utalii) na Gerson Msigwa (Utamaduni, Sanaa na Michezo) na kuhudhuriwa na watendaji wa sekta hizo wameazimia kuainisha maeneo muhimu ya kushirikiana ili yatumike kutangaza utalii ambapo pia imeundwa timu ya kuandaa mkakati huo na bajeti yake.

Akifungua kikao hicho Dkt. Abbasi amefafanua kwamba kutokana na kushabihiana kwa malengo ya Wizara hizi mbili Viongozi Wakuu wa Taifa wakiwemo Mhe. Rais, Mhe. Makamu wa Rais na Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameelekeza kuwepo kwa ushirikiano katika uendeshaji wa shughuli za sekta kwa manufaa ya taifa.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia katika Tamasha la Utamaduni Viwanja vya Red Cross Mwanza Septemba 8, 2021, alisisitiza, utamaduni ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato, hivyo ni muhimu kutekeleza kwa nguvu kubwa katika kukuza utalii wa kitamaduni.

“Utalii wetu umejikita zaidi kwenye maliasili, wanyamapori, misitu, fukwe milima na mambo mengine, na hii pia inachangia watalii wanaokuja nchini kukaa siku chache; idadi ya siku ambazo watalii hukaa nchini ni ndogo mno, lakini tungekuwa na matamasha ya aina hii wangezunguka na kuona na kujifunza. Na hii ndio maana, Serikali imejipanga kuongeza wigo wa vivutio vya utalii, ukiwemo utalii wa kiutamaduni”. Alisema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amesema Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo zina wadau na matukio maarufu wenye mvuto na ushawishi mkubwa katika jamii ndani na nje ya nchi na hivyo kutoa fursa kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Aidha, amefafanua kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya asili na vya kitamaduni kama vile fukwe za Bahari ya Hindi, maziwa, mito, milima, mabonde, wanyamapori, misitu mikubwa ya asili, tamaduni za kipekee kutoka kwa jamii zaidi ya 120

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *