MHE. SIMBACHAWENE AAGIZA SIMBA KURIPOTI TAKUKURU TUHUMA ZA RUSHWA MCHEZO WAKE DHIDI YA YANGA

Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Klabu ya Simba kama imebaini vitendo vya rushwa katika mchezo wake dhidi ya Yanga uliochezwa Novemba 5, 2023 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam itoe taarifa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU), Manispaa ya Temeke ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Mhe. Simbachawene amesema hayo Novemba 8, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu Swali la Nyongeza la Mhe. Festo Sanga aliyetaka kujua Kauli ya Serikali kuhusu Klabu ya Simba kuwasimamisha baadhi ya wachezaji wake kwa madai ya kuwepo kwa viashiria vya rushwa katika mchezo huo.

Awali akijibu Swali hilo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Wizara kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekua ikipinga vitendo vya rushwa michezoni ambapo kwa kushirikiana na TAKUKURU wamekua wakitoa Elimu kuhusu suala hilo na kwamba tayari wameaanzisha Kampeni inayoitwa ” Kataa upangaji wa Matokeo, Linda hadhi ya Mpira wa Miguu” ambayo inaendelea kuleta matokeo mazuri pia kushirikiana na wadau wengine wa michezo vikiwemo Vilabu husika kupinga vitendo hivyo.

Katika hatua nyinginime, Mhe. Mwinjuma amesema Serikali inaendelea kukarabati Viwanja Saba katika majini ya Tanga, Morogoro, Dodoma, Arusha ili viweze kuwa na hadhi nzuri itakayokidhi kuchezewa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania.

Aidha, Mhe. Mwinjuma amesema programu mbalimbali za TFF katika kuendeleza Mpira wa Miguu ikiwemo Ligi za vijana, Ligi za Daraja la kwanza hadi la nne ambazo zote zinalenga kukuza vipaji, kuendeleza vijana katika kushiriki michezo na kujiunga na Klabuza ndani na nje ya nchi pamoja na Timu za Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *