KATIBU MKUU MSIGWA ATAKA WATUMISHI WAONGEZE UBUNIFU

Na Shamimu Nyaki

Katibu Mkuu wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amewataka Watumishi wa Wizara hiyo waongeze ubunifu katika utekekezaji wa Majukumu yao ili Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ziendelee kuwanufaisha wananchi.

Katibu Mkuu Gerson Msigwa, ametoa rai hiyo Novemba 10, 2023 Mtumba Jijini Dodoma alipokutana na kufanya kikao na watumishi wa wizara hiyo, ambapo amewataka wawe mstari wa mbele katika kubuni, kuanzisha na kusimamia matukio mbalimbali ya michezo yenye lengo la kuinua ari ya wananchi kupenda michezo.

Ametoa wito kwa watendaji na watumishi wa wizara hiyo waongeze ubunifu katika kuanzisha programu zenye lengo la kuibua miradi itakayoendana na wakati uliopo kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta hiyo.

“Leteni mawazo mapya kwa kuandika miradi, ikibidi shirikianeni na Sekta binafsi ili Wizara yetu iwe na vyanzo vya mapato nje ya Bajeti ili tuweze kutekeleza vyema kazi zetu, ikiwemo kutoa furaha kwa watanzania na kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na watu kutokufanya mazoezi” amesisitiza Bw. Msigwa.

Katika hatua nyingine amewasisitiza watumishi hao waendelee kudumisha upendo, ushirikiano umoja katika utendaji wa kazi ili malengo ya Serikali kwa Wizara hiyo katika kuendeleza Sekta za Utamaduni, Sanaa na michezo yaweze kutimia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *