CP WAKULYAMBA ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TAWA, AIPONGEZA NA KUHIMIZA KULINDA MALIASILI ZA NCHI KWA UDI NA UVUMBA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba ameeleza kuridhishwa kwake na Kasi ya utendaji mzuri wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA katika kulinda rasilimali za nchi bila kujali vipingamizi vinavyo jitokeza katika utekelezaji wa majukumu hayo ya kitaifa Ameyasema hayo wakati wa ziara yake Makao Makuu ya ofisi za TAWA Mkoani Morogoro alipokuwa akiongea na menejimenti ya Taasisi hiyo Novemba 29, 2023 ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya, kazi nzuri sana sana mnayoifanya achilia mbali changamoto mbalimbali lakini kiukweli kazi mnaifanya” amesema

Kamishna Wakulyamba amesema lengo la kwanza la kuanzishwa kwa Taasisi za uhifadhi nchini hususan Taasisi za kijeshi za uhifadhi, ni kuimarisha ulinzi wa maliasili hivyo kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii amezielekeza Taasisi hizo kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi kwa nguvu zote ili ziweze kutumika kwa manufaa na lengo la  utalii

“Lazima tulinde maliasili zetu kwa udi na uvumba, ndiyo kazi tuliyokabidhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba,  hatujapewa kwa hisani ya mtu tumepewa kwa mujibu wa Katiba na sheria za bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ” amesisitiza Kamishna Wakulyamba Pia amesisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ni Wizara ya  kibiashara na kimkakati hivyo Mamlaka inapaswa kujidhatiti katika kuimarisha vitengo vya utalii na masoko kwa lengo la kuiingizia Serikali mapato.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa TAWA kwa Mwaka 2022/23 kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Asha Kilili amesema mojawapo ya mafanikio ya TAWA kwa Mwaka huo wa fedha ni kutoa elimu na mbinu rafiki za kujikinga na madhara yanayosababishwa na Wanyamapori Wakali na Waharibifu kwa wananchi zaidi ya Laki nne katika jumla ya vijiji 1,319 ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa vituo 16 vya askari wa kudhibiti wanyama hao na kuweka vitendea kazi ikiwemo pikipiki 50

Sambamba na hilo Asha Kilili amesema TAWA iliweza kufukuza jumla ya tembo takribani 554 kwa helkopta katika wilaya za Nachingwea, Liwale, Same na Bunda ikiwa ni pamoja na kufunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa makundi ya tembo 8 katika wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwea

Aidha amesisitiza kuwa TAWA itaendelea kuongeza ubunifu na mbinu mbalimbali katika kukabiliana na matukio ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu, ulinzi wa rasilimali za Wanyamapori pamoja na kuongeza mapato

Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *