Uholanzi, kupitia Shirika lake la Invest International, imeipatia Tanzania, msaada wa euro milioni 30, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 82 za Tanzania, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Bonde la Msimbazi, Jijini Dar es Salaam.
Mkataba wa msaada huo umetiwa saini jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Tanzania, na Balozi wa Serikali ya Ufalme ya Uholanzi, Mhe. Wieber De Boer.
Dkt. Mwamba katika hotuba yake alisema, fedha hizo ni sehemu ya gharama ya Mradi huo wa Uendelezaji Bonde la Msimbazi, utakaogharimu dola za Marekani milioni 260, ambapo kati ya kiasi hicho, Benki ya Dunia itatoa dola za Marekani milioni 200 na Serikali ya Hispania itatoa euro milioni 30 kama mkopo nafuu.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaondoa changamoto ya mafuriko ynayotokea kila mwaka katika Bonde hilo kwa kujenga njia za kuelekeza maji, kujenga kingo za mto Msimbazi, kudhibiti kujaa mchanga katika mto, na kudhibiti mmomonyoko wa udongo.
“Fedha hizo pia zitatumika kupanua na kujenga daraja la juu (flyover) eneo la Jangwani, ili kuepusha madhara ya mafuriko na kubadilisha eneo oevu la Jangwani kuwa eneo la vivutio vya Jiji la Dar es Salaam” alisema Dkt. Mwamba
Aliongeza kuwa mradi huo pia utawezesha kuhamishwa kwa Ofisi za Mabasi ya Mwendokasi kutoka eneo la Jangwani linaloathirika na kujaa maji kila mwaka kwenda eneo la Ubungo Maziwa.
“Mafuriko katika eneo la Jangwani yameigharimu Serikali kiasi kikubwa katika eneo la mapato na familia zinazoishi karibu na eneo la Bonde la Msimbazi ambazo zimekuwa zikiathirika majira ya mvua yakisasbabisha kufungwa kwa barabara kuelekea katikati ya Jiji ambayo ni kitovu cha biashara” alisisitiza Dkt. Mwamba.
Aidha, Dkt. Mwamba aliishukuru Uholanzi kwa kuchochea maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na nchi hiyo ikiwemo ukarabati wa huduma za uchunguzi wa kimatibabu katika hospitlai 34 katika mikoa 21 Tanzania (euro milioni 11.5), mradi wa kudhibiti taka jijini Dar es Salaam (euro 840,000), ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (euro milioni 14) na msaada wa euro milioni 20 kwa ajili ya mradi wa umeme vijijini katika wilaya za Ngara, Biharamulo na Mpanda.
Kwa upande wake Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber De Boer, amesema kuwa mradi wa Uendelezaji Bonde la Msimbazi ni muhimu kwa uchumi na maisha ya wakazi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakikumbwa na adha ya mafuriko kila mara na kuhatarisha maisha yao.
Alisema pia kuwa mradi huo si tu kwamba utadhibiti mafuriko na kujaa maji katika eneo husika, bali pia utaleta mandhari nzuri ya Jiji la Dar es Salaam na kuvutia watalii kutokana na miundombinu muhimu itakayojengwa katika eneo hilo. “Ni muhimu wananchi wa Dar es Salaam na maeneo mengine wauunge mkono mradi huo kwa kuwa umekuja kutatua adha kubwa waliyokuwa wanaipata na kwa kuwa utakuwa chanzo kimoja wapo cha kukuza uchumi wa nchi” Aliongeza Balozi De Boer
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), Bw. Victor Seif, alisema kuwa Wakala wake pamoja na Tanroads ambao ndiyo watekelezaji wa mradi huo, watafanya kila njia kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kama ulivyopangwa na kwa wakati ili kuwaletea wananchi manufaa.