Tanzania na Sweden, kupitia Taasisi ya Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kimaendeleo la Sweden (SIDA), zimesaini Mkataba wa Msaada wenye thamani ya dola za Marekani milioni 84 sawa na takriban shilingi bilioni 210, kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa Programu ya Kuimarisha Kada ya Ualimu nchini. Mkataba huo umetiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Charlotta Ozaki Marcias.
Dkt. Mwamba, alifafanua kuwa katika fedha za msaada huo, dola za Marekani milioni 29.3 zitatumika kuboresha mchakato wa ukusanyaji data za elimu; kuboresha elimu ya walimu, ajira, maendeleo endelevu ya kitaaluma, motisha, na uwajibikaji. Aidha, alisema kuwa dola za Marekani milioni 54.8 zitatumika kufadhili shughuli zinazotegemea matokeo, zikiwa na lengo la kuinua nguvu kazi ya walimu, usawa wa kijinsia, ushirikishwaji, na mazingira ya ufundishaji na kujifunza shuleni ili kuchochea mabadiliko ya kimageuzi kwa kada ya ualimu ambapo itaongeza ufanisi katika mfumo wa elimu ya msingi.
Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkataba huo utaongeza jumla ya misaada kutoka GPE nchini Tanzania kufikia dola za Marekani milioni 309, sawa na takriban shilingi bilioni 773 na kwamba fedha hizo zimekuwa nguvu inayoendesha mabadiliko chanya katika mfumo wa elimu, ukigusa maisha ya wengi. “Tunashukuru kwa michango ya kipindi kilichopita, ambapo Tanzania ilipata misaada kupitia fedha za GPE jumla ya dola za Marekani milioni 225 sawa na takriban shilingi bilioni 562 zilizotumika kugharamia utekelezaji wa programu ya kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa awamu ya kwanza kuanzia 2013 – 2018 na awamu ya pili kuanzia 2019 – 2024” Alisema Dkt. Mwamba Dkt. Mwamba aliihakikishia Sweden, dhamira ya Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi hiyo, GPE na Washirika wote wa Maendeleo ili kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Marcias, alisema kuwa tangu Tanzania ijiunge na Taasisi ya Ushirikiano wa Elimu Duniani (Global Partneship for Education-GPE), mwaka 2013, sekta ya elimu imeboreshwa ikiwemo kupungua kwa msongamano wa wanafunzi wa shule za msingi madarasani kutoka wastani wa wanafunzi 113 hadi kufikia wanafunzi 50. Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwa wakala wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kutimiza wajibu wake wa kuboresha mifumo ya elimu nchini ili kuyanufaisha makundi ya walimu kwa kuwajengea ujuzi, maarifa, kuwapa motisha, ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu. Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bi. Laura Fringent, aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga katika maendeleo ya sekta ya elimu na kuahidi kuwa Taasisi yake, itaendelea kutoa mchango wa kuboresha mazingira ya walimu nchini ili kuboresha zaidi elimu kwa faida ya maendeleo ya Taifa. Awali, akitoa maelezo ya mpango huo wa kuboresha elimu kupitia walimu unaofadhiliwa na Taasisi hiyo ya Global Partnership for Education, Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI, Profesa James Mdoe, alieleza kuwa msaada huo utaimarisha zaidi nguvu kazi ya walimu katika kipindi cha miaka minne ijayo kuanzia mwaka 2023/2024 hadi 2026/2027.