SIMBA SC YAKABIDHI MSAADA KWA WAHANGA WA MAPOROMOKO YA UDONGO KATESH

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro leo Desemba 5, 2023 jijini Dar es Salaam amepokea vyakula na bidhaa mbalimbali ikiwemo sukari, sabuni, unga wa ngano na Maji kutoka kwa uongozi wa klabu ya Simba ikiwa ni msaada kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea Katesh wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Akizungumza mara baada ya kupokea bidhaa hizo Mhe. Ndumbaro ameipongeza klabu ya Simba kwa kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msaada huo ambao unaenda kusaidia wahanga hao.

Aidha, Mhe. Ndumbaro amevitaka vilabu vingine nchini kuiga mfano huo kwa kutoa msaada kwa jamii ya wana Hanang waliokumbwa na majanga hayo usiku wa kuamkia Desemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu, kuharibu miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo Barabara pamoja na makazi ya watu wa eneo hilo.

Mhe. Waziri Dkt. Ndumbaro ametoa pole kwa wananchi wa Katesh na watanzania kwa ujumla kwa athari zilizotokea wilayani hanang na kuwatakia matibabu mema majeruhi ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *