KATIBU MKUU GERSON MSIGWA AIPONGEZA COSOTA KWA UTAFITI WA MCHANGO WA HAKIMILIKI KATIKA PATO LA TAIFA

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa ameipongeza Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kwa kuanza mchakato wa kufanya utafiti wa kuhuisha taarifa ya utafiti wa mwaka 2012 kuhusu mchango wa Hakimiliki katika pato la Taifa.

Msigwa ametoa pongezi hizo Leo Desemba 06,2023 katika kikao chake na Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki COSOTA Bi. Doreen Anthony Sinare kilichofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma ambapo pia mtendaji huyo ametoa taarifa ya utafiti uliofanyika mwaka 2012 na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) na COSOTA na BRELA.

“Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuwa ikichangia sana kwenye pato la Taifa ila kumekuwa na shida ya kuwa na Takwimu sahihi ambazo zinaonesha namna gani sekta hizo zinachangia katika pato la Taifa. Hii ni moja ya tafiti muhimu itakayosaidia kuwa na majibu sahihi ya tasnia zinazohusu Hakimiliki na mchango wake “amesema Msigwa.

Ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Damas Ndumbaro mara kwa mara wamekuwa wakisisitiza kupatikana kwa taarifa za namna sekta za Wizara zinavyochangia katika pato la Taifa ikiwepo suala la ajira.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa COSOTA Doreen amesema kuwa lengo la utafiti huo ni kuhuisha taarifa za 2012 zitakazowezesha kuanzisha kwa utoaji wa tuzo kwa wale watakaokuwa wametoa mchango mkubwa katika pato la Taifa.

“Katika kikao cha COSOTA na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kilichofanyika Desemba 5, 2023 tumekubaliana kuendelea na kazi hii kwa kushirikisha Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO), BRELA, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambayo imeahidi kutoa ushirikiano ili kufanikisha utafiti huu,” alisema Doreen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *