SERIKALI imeendelea kupokea misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa ajili ya kusaidia waathirika wa maafa ya mafuriko na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang’ mkoani Manyara. Akipokea misaada hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama hii leo Disemba 07, 2023 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki ameishukuru taasisi ya TATO (Tanzania Association of Tour Operators) kwa kuungana na Serikali katika kusaidia waathirika wa maafa yaliyotokea tarehe 03 Disemba 2023 mkoani humo huku akiwasihi wadau kuendelea kujitokeza kuchangia kwa hali na mali ili kuendelea kurejesha hali kwa wananchi hao.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu nimepokea misaada hii na tunawashukuru sana kwa namna mlivyoungana na Serikali, nichukue nafasi hii kuwaomba wadau wengine kuendelea kuungana na Watanzania wenzetu ili kuona namna tunavyoweza kuwasaidia,” alisema Mhe. Kairuki.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau kujitokeza kwa kuzingatia ukubwa wa mahitaji uliopo ikiwemo vifaa vya ujenzi ili kutoa unafuu kwa waathirika wa tukio hilo.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi ametoa shukrani kwa misaada hiyo huku akieleza kuwa maji yaliyokabidhiwa yatasaidia kuendelea kujilinda na magonjwa ya milipuko kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa afya zao.
“Asanteni sana TATO kwa kuona umuhimu wa kutukimbilia, na mmetoa misaada itayosaidia ndugu zetu waliopata maafa haya na hii inatupa nguvu katika kurejesha hali huku tukiendelea kuungana pamoja kwa lengo moja la kuwasaidia,” alisema.
Naye, Bw. Wilbord Chambulo ambaye ni Mwenyekiti wa TATO Arusha (Tanzania Association of Tour Operators) akieleza misaada waliyokabidhi ikiwemo unga wa ngano tani kumi, maji ya kunywa lita 37,800 na mafuta ya kula lita 2000.
Tumekabidhi na tutaendelea kujitoa ila chama kimeona umuhimu wa kuungana na Watanzania wenzetu kwa tukio hili zito la maafa, sisi TATO tutaendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia ni ndugu zetu na maafa haya yametokea kama jambo la dharura hawakulitarajia,”alisema.