DKT. NCHEMBA AFAFANUA UKOMO WA BAJETI 2024/25

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akizungumza wakati wa hafla ya Uwekaji Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Taaluma la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Kampasi ya Dodoma, katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, ambapo alitumia jukwaa hilo kufafanua ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2024/25.

Na Saidina Msangi na Joseph Mahumi, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano Afrika kwa kutimiza viashiria vya Malengo ya Milenia ambapo imefanya vizuri katika sekta za Afya, Elimu, Maji. 
Dkt. Nchemba alitoa ufafanuzi huo wa ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2024/25, wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika jengo la Taaluma la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), jijini Dodoma.
Alisema kuwa katika makadirio yaliyowasilishwa bungeni Serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi trilioni 49.34 ambapo fedha za maendeleo zilizotengwa ni kiasi cha shilingi trilioni 16.
‘‘Fedha za maendeleo ni trilioni 16, fedha hizi zinatarajiwa kutumika katika Miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji, Elimu ya Msingi na Elimu ya Juu, Ujenzi wa Barabara, Maji, Umeme Miradi ya Afya pamoja na ukamilishaji wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere’’, alifafanua Dkt. Nchemba.  
Alisema kiasi cha fedha kinachotarajiwa kutumika katika uchaguzi ni shilingi bilioni 600 kwa mwaka unaofuata na kwa mwaka huu ni Shilingi bilioni 300 inayoenda kwenye uchaguzi.
‘‘Uchaguzi ni matakwa la kikatiba sio maamuzi ya Serikali bali ni kuhakikisha kuwa matakwa ya kikatiba yanatimizwa hivyo katika bajeti ya Sh. trilioni 49 kiasi kitakachoitumika katika kuendesha uchaguzi kwa mwaka ujao ni shilingi bilioni 300, alifafanua Dkt. Nchemba.
Akifafanua kuhusu fedha zinazotarajiwa kutumika katika maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 linalotarajiwa kufanyika Tanzania Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON ni suala la kujivunia kwani ni heshima kwa Taifa ambapo kiasi kilichotengwa ni Sh. bilioni 200 tu katika bajeti ya shilingi. trilioni 49. 
Akizungumza kuhusu ugharamiaji wa Deni la Taifa Dkt. Nchemba alisema kuwa katika sh. trilioni 49, deni halisi ni shilingi trilioni tano (5) pamoja na riba ambayo haitazidi kiasi cha shilingi trilioni 10. 
‘’Deni lenyewe ni miradi ya maendeleo inayoonekana kama ni ujenzi wa reli ya kisasa, kivuko cha Kigongo Busisi Mwanza, ujenzi wa mabweni ya shule, tumejenga mabweni ya vyuo vikuu karibu kila chuo kimepata kwa mradi mkubwa wa fedha za Benki ya Dunia ili kuwawezesha wanafunzi wakae katika mazingira salama’’,alifafanua Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita zinaonekana kwani fedha za maendeleo yanayotekelezwa yanajitambulisha kwani zimegusa mpaka kwenye maeneo ambayo hayajawahi kupata maendeleo.
‘‘Vijiji ambavyo havijawahi kupata barabara sasa vina madaraja na barabara kuunganisha vijiji na sasa zinaenda kujengwa barabara za kudumu, vituo vya afya vimejengwa kwenye kila makao makuu ya tarafa pamoja na kuweka vitendea kazi ambapo ndani ya miaka mitatu mikoa yote ina CT SCAN ambapo awali zilikuwepo 6 nchi nzima’’, alifafanua Dkt. Nchemba. 

MWISHO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *