KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA MRADI WA UVIKO-19 PUGU KAZIMZUMBWI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na matumizi ya fedha za mradi wa UVIKO-19 za kuboresha miundombinu ya utalii katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi uliogharimu takribani shilingi milioni 579.1

Hayo yamesemwa leo Machi 16, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Najma Giga walipofanya ziara ya kukagua miradi iliyotekelezwa na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika msitu huo

“Kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha za UVIKO-19 hasa katika ujenzi wa kituo cha taarifa za utalii, ukiliangalia lina thamani halisi ya fedha” Mhe. Najma amesisitiza.

Aidha, ameitaka TFS kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kuongeza matangazo ya eneo hilo ili kuvutia watalii wengi zaidi.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa msitu wa Pugu Kazimzumbwi ni muhimu kiikolojia, kiutamaduni na kiuchumi kwa jamii ya Kisarawe, Mkuranga, Dar es Salaam na maeneo mengine.

Pia, amesema kuwa msitu huo una faida katika kulinda vyanzo vya maji na kupatikana kwa hewa safi.

Mhe. Kairuki amefafanua kuwa ili kukuza shughuli za utalii katika msitu huo, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kufungua barabara zaidi za kutembelea watalii na kupanda mimea tiba itakayotumika kama tiba ya asili.

Kwa upande wake Kamishna Uhifadhi wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema fedha za UVIKO-19 zilitengwa kwa ajili ya kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilomita 12 kutoka Kimani- Maguruwe, ujenzi wa lango la kuingilia lenye ofisi, kituo cha taarifa za utalii, ofisi ya malipo, kibanda cha mlinzi na vyoo.

Ziara hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi pamoja na Watendaji na Menejimenti ya Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *