Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakiwasili Kata ya Ibadakuli iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kukagua utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Machi 20, 2024 wakati zoezi la uhakiki wa majina ambayo tayari yametambuliwa na taarifa zao kuingizwa kwenye ramani ya eneo husika.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda wakiangalia zoezi la uwekaji alama wakati Kamati ya PAC ilipokwenda kukagua utekelezaji mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Machi 20, 2024.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe, Japhet Hasunga akiongea na wananchi wa Kata ya Ibadakuli Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kukagua utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Machi 20, 2024.
Na Eleuteri Mangi, Shinganga
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelelezwa na Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi katika Manispaa ya Shinyanga ili kuangangalia hatua zilizofikiwa pamoja na thamani ya fedha iliyotumika kutekeleza mradi huo katika manispaa hiyo.
Hayo yamesemwana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga wakati wa majadiliano mara baada ya kutembelea miongoni mwa maeneo unapotekelezwa mradi huo ikiwemo kata ya Ibadakuli na Kibada ambapo wajumbe wa kamati hiyo walijionea wananchi wakihakiki taarifa zao ambazo zilichukuliwa wakati wa utambuzi na maeneo walipokuwa wanaweka alama za utambuzi wa maeneo (bicorns).
“Tumetembelea maeneo mbalimbali, tumeona wanavyotekeleza huu mradi tumepokea taarifa ya utekelezaji wa mradi na ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Kamati imemwelekeza Katibu Mkuu kuhakikisha wanafikia lengo la kutoa hati miliki za ardhi kwa wananchi ambao vipande vyao vya ardhi vimetambuliwa na kupangwa kulingana na matumizi ya ardhi hapa Shinyanga na kuhakikisha malengo ya mradi huo katika manispaa ya Shinyanga yanatekelezwa kabla ya kufika mwezi Juni 2024” amesema Mhe. Hasunga.
Akiongea na wananchi wa kata ya Ibadakuli iliyopo Manispaa ya Shinyanga, Makamu Mwenyekiti kamati ya PAC Mhe. Hasunga amesema kumalizika kwa migogoro ya ardhi kupitia mradi huo wananchi wa manispaa ya Shinyanga kutatoa fursa wananchi kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo yao ikiwemo kujenga nyumba katika maeneo wanayomiliki kwa kuwa na hati miliki za ardhi.
“Ukiwa na hati ya kumiliki eneo hapo hakuna mtu atakayekuondoa tena, hapo ndipo utakapoona manufaa ya kumiliki ardhi, hiyo hati itakusaidia mambo mengi. Unaweza kwenda benki kupata mikopo kufanya shughuli zako za maendeleo, utajenga nyumba na kufanya shughuli nyingine za maendeleo ukiwa na hati yako. Bila hati, eneo sio lako”
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amewashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa ushirikiano wanaoendelea kupata katika kutekeleza majukumu yao na wamepokea maelekezo na ushauri wa kamati na kuahidi kuyafanyia kazi kama walivyoelekeza.
Aidha, Katibu Mkuu Mhandisi Sanga ameongeza kuwa wameijulisha Kamati hiyo kuwa kazi ya Mradi wa LTIP inayoendelea Manispaa ya Shinyanga inaendelea vizuri na imefikia asilimia 51 ya utekelezaji wa mradi na kazi hiyo itakamilika katika halmashauri ya Shinyanga kama ilivyoelekezwa na Kamati hiyo.
Akifafanua kwa Kamati hiyo Mratibu wa Mradi wa LTIP Bw. Joseph Shewiyo amesema kwa Manispaa ya Shinyanga mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha Shilingi 1,417,411,000 ambapo Shilingi 1,396,000,000 imepangwa kwenye shughuli za urasimishaji na Shilingi 21,411,000 zimepanwa kujenga alama za msingi za upimaji na hadi sasa Shilingi 451,749,000 zimtumika kwenye kazi ya utambuzi, upangaji na upimaji, kununua vifaa, ujenzi wa alama za msingi 10 na elimu kwa umma.