TANZANIA NA IVORY COAST ZAINGIA RASMI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KWENYE SEKTA YA MICHEZO

Na, Brown Jonas – WUSM, Dar es Salaam.

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeingia makubaliano ya ushirikiano na Wizara ya Michezo ya Ivory coast katika masuala mbalimbali ya uendelezaji wa Sekta ya michezo.

Makubaliano hayo yameingiwa leo Aprili 21, 2024 Jijini Dar Es Salaam ambapo Naibu Waziri Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa upande wa Tanzania Mhe. Hamis Mwinjuma amesaini makubaliano hayo kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro huku Ivory Coast aliyesaini makubaliano hayo ni Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Mhe. Adjé Silas.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mhe. Mwinjuma amesema makubaliano hayo yatajikita kwenye uandaaji wa miundombinu ya michezo, uandaaji wa timu kuelekea michuano ya AFCON 2027 itakayofanyika nchini Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

“Sisi na Ivory Coast tutashirikiana kwenye maeneo tofauti kwa kuwa tunafanana kwenye mazingira mengi, hivyo ni bora kujifunza kwa mtu unaefanana nae kuliko kwenda kuchukua watu wa dunia ya kwanza waje kukufundisha vitu ambavyo itakua ngumu kuvifanya” Amesisitiza Mhe. Mwinjuma.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Bw. Gerson Msigwa, Naibu katibu Mkuu Dkt. Suleiman Serera Kaimu Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya Michezo Bw. Ally Mayay, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msitha, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa Dkt. Kedmon Mapana pamoja na Maofisa wa nchi hizo mbili.

Picha ya pamoja

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *