Na Eleuteri Mangi
Waendesha baiskeli wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wameibuka mabingwa wa mchezo wa kuendesha baiskeli kwa wanaume na wanawake katika Michuano ya Michezo ya Mei Mosi 2024 inayoendelea kupamba moto jijini Arusha.
Kwa wanaume ambao wameendesha baiskeli kwa KM 55, James Shigela ametumia muda wa saa 1:27 na Alavuya Michael Ntalima kwa wanawake ambao waliendesha baiskeli kwa umbali wa KM 35 ametumia saa 1:05.
Nafasi ya pili kwa wanaume imekwenda kwa Hassan Ligoneko kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye alitumia saa 1:30, nafasi ya tatu imekwenda kwa Stevine Sanga kutoka Hospitali ya Ocean Road ambaye ametumia saa1:30:14 wakati kwa upande wa nafasi ya pili kwa wanawake imekwenda kwa Scholastica Asili kutoka Wizara ya Uchukuzi ambaye ametumia saa 1:05:25 na nafasi ya tatu imechukuliwa na Ester Chacha kutoka Wizara ya Afya ambaye ametumia saa 1:28.
Michezo hiyo mefikia hatua ya robo fainali ambayo ni mpira wa miguu, netiboli, kamba wanaume na wanawake pamoja na mpira wa wavu wannaume na wanawake.
Baadhi ya timu zilizofuzu hatua hiyo katika mpira wa miguu ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambao waliwafunga Wizara ya Fedha magoli 5:0, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wamewafunga timu ya Wizara ya Afya magoli 2-0, timu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wameifunga timu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora magoli 2-0 na timu ya TANROADS wamewafunga Meru DC 3-1.
Katika mchezo wa Netiboli, timu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI wamewafunga timu ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) jumla ya magoli 103-0, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wamewafunga Shirikanla Viwango Tanzania (TBS) magoli 69-7, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wameibuka kidedea kwa kuwafunga NSSF kwa magoli 30-20, Ofisi ya Rais Ikulu wamewafunga Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora magoli 37-20.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Aprili 30, 2024 yakifuatiwa na maadhidhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.