TIC IMEKUWA INJINI KUTEKELEZA MAONO YA RAIS DKT. SAMIA – MAJALIWA.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi na wafanyakazi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kuwa injini ya kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muuumgano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga Tanzania yenye mvuto kwa wawekezaji wote.

“Hatua ambayo nchi yetu imefikia kwa sasa, inaondoa shaka kwa wawekezaji na imeendelea kuthibitisha kuwa nchi yetu ni salama kwa wote waliotayari kuwekeza mitaji yao. Endeleeni kuwa wabunifu, kuimarisha utoaji huduma na kukidhi mahitaji ya ushindani katika masoko ya uwekezaji.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imeleta mageuzi makubwa kwa kufanya maboresho mbalimbali katika mifumo, sera na sheria ili kuboresha mazingira ya biashara na kuvutiauwekezaji hapa nchini.

“Kipindi cha miaka mitatu ya mageuzi kimedhihirisha matokeo ya dhamira njema ya Mheshimwa Rais katika kukuza diplomasia ya kiuchumi na kujenga mazingira bora na rafiki ya uwekezaji hapa nchini.”

Ameyasema hayo leo (Jumapili Aprili 28, 2024) wakati alipokuwa akifungua Semina Maalum ya uwekezaji kwenye kilimo iliyoandaliwa na benki ya CRDB katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki, Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imeimarisha utoaji huduma kwa wawekezaji kwa kuimarisha Kituo cha Utoaji wa Huduma za Mahali Pamoja kilichoko TIC ambapo kwa kwa sasa taasisi 14 za Serikali zinatoa huduma katika Kituo cha mahali pamoja.

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Wizara ya Kazi, Wizara ya Ardhi, Uhamiaji, NIDA, NEMC, TRA, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Madini, BRELA, TBS, TMDA, OSHA, TANESCO na TIC yenyewe.

“Hatua hiyo imetekelezwa sambamba na uboreshaji wa Mfumo wa Kusajili Miradi ya Uwekezaji yaani Tanzania Investment Window (TIW) na kumwezesha mwekezaji kusajili mradi wake ndani ya siku moja hadi tatu iwapo amekamilisha nyaraka zote muhimu tena akiwa mahali popote duniani. Hii ni hatua kubwa na muhimu iliyoondoa ukiritimba usiokuwa wa lazima.”

Kwa Upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Sekta ya uvuvi imeendelea kuimarika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ikiwa ni sambamba na ugawaji wa boti za kisasa za uvuvi pamoja na vizimba vya kufugia samaki.

Naye, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Shaaban Ali Othman, amesema Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imenufaika na uwezeshaji unaoganywa na benki ya CRDB ambayo ka kiasi kikubwa imewanufaisha wavuvi na wakulima wa zao la mwani ambalo uzalishaji wake umeongezeka.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Sera nzuri zilizowekwa na Serikali katika sekta ya kilimo zimewezesha wawekezaji wengi kuwekeza katika Sekta hiyo, ikiwa ni sambamba na ongezeko kubwa la ajira kwa vijana, na kutanabaisha kuwa mradi wa BBT umekuwa mfano bora wa utenegezaji wa ajira na njia ya kuonesha fursa zilizopo katika Sekta ya kilimo.

Naye, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, Gilead Teri, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa Wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutoa ardhi kwa ajili ya maeneo ya uwekezaji.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Benki hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza wawekezaji kwa kuendelea kuwawezesha mitaji pamoja na kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji Nchini.

Semina hiyo imewakutanisha wadau wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi pamoja nawazalishaji wa zana za kilimo na mifugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *