Na Mwandishi maalum.
Wanafunzi waliohama kutoka shule mbalimbali zilizopo tarafa ya Ngorongoro na kuhamia katika shule zilizopo Kijiji cha Msomera wameishukuru serikali kuwahamisha kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi na kuwapeleka kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Baadhi ya wanafunzi hao kutoka tarafa ya Ngorongoro na sasa wanasoma katika shule ya Msingi Msomera na Sekondari ya Dkt. Samia Suluhu Hassan wamesema hali katika shule zilizopo katika tarafa ya Ngorongoro ilikuwa ni mbaya kutokana na umbali na kuzungukwa na wanyama wakali na ukungu hasa nyakati za asubuhi.
Mwanafunzi Soiti Lemurwa ambaye kwa sasa anasoma katika shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan anaeleza kuwa alipokuwa Ngorongoro alikuwa hana amani ya kushiriki katika masomo kutokana na kuogopa wanyama pori na wakati mwingine ilibidi atoroke shule ili kulinda uhai wake.
“Tunaishukuru serikali kwa kutuondoa hifadhini Ngorongoro, ilikuwa ni vigumu kwetu kusoma kwa furaha kutokana na idadi ya wanyama pori inavyoongezeka kila siku, uhai wetu ni muhimu kuliko kitu chochote kile kwani hapa Msomera tunasoma kwa amani”,alisema Lemurwa.
Naye Mathayo Saruni anaeleza kuwa maisha ya Ngorongoro yalikuwa na changamoto nyingi kielimu na alishakata tamaa kutokana na kuongezeka kwa wanyama pori hasa simba na chui hivyo uamuzi wa wazazi wake kuhama katika tarafa hiyo umempa ari ya kusoma kwa bidi.
“Kwa kweli hali ilikuwa mbaya,Watoto tulikuwa tunawaza jinsi ya kwenda na kurudi shuleni kila tunapofikiria wanyama pori,kwetu sisi ilikuwa tunajiona ni kama Watoto tofauti na wenzetu wanaosoma maeneo mengine nchini Tanzania”,alisema.
Kwa upande wake mwanafunzi Elizabeth Napoiky aliwashangaa watu wanaowashawishi wazazi wao wasihame na kukimbilia kwenye jumuiya za kimataifa na kusema kuwa wao ni watu wa asili ya Ngorongoro na kueleza kwamba kitendo hicho wanakipinga.
“Tunawashangaa baadhi ya wazazi wetu wanaotutumiwa kupata fedha kwa kisingizio cha sisi ni kivutio vha utalii,hilo jambo kwa sasa tunalipinga kwani sisi ni binadamu sio kivutio cha utalii na tuna haki ya kupata elimu kama walivyo Watoto wenzetu nchini Tanzania”,alisema Elizabeth.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Samia Suluhu Hassan Charles Andrea aliipongeza serikali kutokana na namna ya miundo mbinu ya kutoa elimu ilivyo bora katika Kijiji hicho.
Mwalimu Andrea amesema shule yake ni bora ukilinganisha na shule nyingi nchini Tanzania kutokana na kujengwa katika mazingira ya kisasa na ikiwa na kila kitu ikiwemo kompyuta za kufundishia pamoja na wanafunzi wote kuwa na uwezo wa kupata mtandao wakati wakitumia kompyuta hizo.
Serikali kwa sasa inatekeleza mpango wa kuwahamisha wananchi wanaoishi katika tarafa ya Ngorongoro kwa hiyari kutokana na wananchi hao kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo kuokoa maisha yao kutokana na ongezeko la wanyama wa kali ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.