Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuendesha Mkutano wa Kimataifa wa Nishati safi ya Kupikia kwa Afrika utakaofanyika Paris, Ufaransa tarehe 14 Mei 2024.
Ushawishi mkubwa wa Rais Samia kuifanya nishati safi kuwa ajenda ya kipaumbe Kimataifa imepelekea kupata mwaliko wa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (International Energy Agency), Dkt. Fatih Biro.
Mkutano huo una jumla ya wenyeviti wanne, wakiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati, Dkt. Fatih Birol; Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Jonas Støre na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Leo Mei 11, 2024 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amesema mwaliko wa Rais Samia unatokana na kuutambua mchango wake katika kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwa championi katika kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kupikia na athari zake. Zaidi ni kulinda mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huu una malengo ya kulifanya suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa la kipaumbele katika ajenda ya kimataifa, kuainisha mabadiliko madhubuti za kisera zitakazoharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, na kutoa fursa ya washiriki kutoa ahadi za kifedha, sera na ubia ili kufikia azma ya kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mwishoni mwa mwaka 2023, katika Mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) Rais Samia alizindua Programu ya Nishati Safi ya Kupikia ya Kusaidia Wanawake Barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme – AWCCSP) ambayo ilipokelewa vyema kimataifa na sasa utekelezaji wake ukiendelea.
Mkutano huu unatarajiwa kujumuisha watu zaidi ya 900 wakiwemo wakuu wa nchi, taasisi na makampuni ya kimataifa yanayohusika na nishati safi ya kupikia.
Pembezoni mwa mkutano huo, Rais Samia atafanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron Ikulu ya Elysee.