MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO YAVUNJA REKODI WANAFUNZI WAPATAO 1,986 WASOMESHWA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24.

Na Mwandishi wetu.

Jumla ya wanafunzi 1,986 wanasomeshwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika hatua mbalimbali za elimu kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka huu 2024 ambapo hadi kufiikia mwezi Aprili tayari zadi ya shilingi bilioni 1.3 zimetumika kwa zoezi hilo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha WATETEZI kaimu meneja wa Uhusiano kwa Umma wa NCAA Bw. Hamis Dambaya amesema katika idadi hiyo ina jumla ya wanafunzi wapya 185.

Amesema kuwa zoezi la kuwapata wanafunzi hao hufanywa na Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro na mchakato wa kuwachagua huzingatia familia zisizokuwa na uwezo na viwango vya ufaulu vilivyowekwa na mamlaka za elimu nchini na zoezi hilo hufanyika mara tu mamlaka inapopata bajeti yake kwa mwaka husika.

“Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro huwajibika kwa kutoa fedha kulingana na bajeti mara baada ya kupata idadi ya wanafunzi na fedha hizo hupelekwa halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ili iweze kuwalipia wanafunzi hao na hivyo hakuna fedha inayolipwa moja kwa moja na mamlaka kwenda mwanafunzi, shuleni au vyuoni”,alisema bwana Dambaya.

Kuhusiana na taarifa kwamba kuna wanafunzi ambao wamekataliwa kusomeshwa na mamlaka hiyo bwana Dambaya amesema kuwa taarifa hizo ni uzushi kwa kuwa idadi ambayo mamlaka ililielekeza baraza kuleta majina yao kwa mwaka huu wa fedha ni wanafunzi 185.

“Katika barua yetu ya tarehe 10 Oktoba 2023 tuliwaelekeza Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro kutuletea majina ya wanafunzi 185 katika viwango tofauti vya elimu lakini kwa upande wa vyuo vya kati baraza lilileta wanafunzi 110 kinyume kabisa na idadi iliyotakiwa ya wanafunzi 55 jambo ambalo halikuwa sahihi,”alisema bwana Damnaya.

Dambaya aliwataka wanafunzi wote ambao wanasomeshwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufuata taratibu pale wanapopata changamoto katika malipo yao mbalimbali kwa kuwasiliana na halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ambao wanawajibika katika masuala yote ya ufuatiliaji wa fedha hizo za ufadhili.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilisitisha kupeleka fedha Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro kuanzia mwaka wa fedha 2020/21 na kuzipeleka fedha hizo halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ili kurahisisha uratibu na usimamizi wa fedha hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *