Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akimkabidhi vipeperushi vyenye taarifa mbalimbali kuhusu elimu ya fedha Bi. Ivona Gasper baada ya kumalizika kwa semina ya utoaji elimu kwa wananchi iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akizungumza wakati wa semina ya utoaji elimu kwa wananchi iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Baadhi ya wananchi walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakifuatilia makala yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba, mikopo, maandalizi ya kustaafu na nyinginezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akifafanua jambo wakati wa semina ya utoaji elimu kwa wananchi iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Baadhi ya wananchi walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakiangalia makala yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba, mikopo, maandalizi ya kustaafu na nyinginezo iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Na. Josephine Majula, WF- Kagera
Wananchi wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwafikishia huduma ya elimu ya fedha itakayowakomboa kiuchumi na kuwaepusha na upotevu wa fedha.
Shukrani hizo zimetolewa na wananchi hao baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata elimu hiyo, Bi. Ivona Gasper Mfanyabiashara alisema kuwa elimu aliyoipata ataenda kuwaelimsha wengine ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha.
“Tunaiomba Serikali iendelee kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wake na kuhakikisha inawafikia watu wote nchi nzima kwa sababu wananchi wengi wanapoteza fedha kwa kukosa elimu” alisema Bi. Gasper.
Mwelimishaji Rika Ngazi ya Jamii Bi. Jackline Petro, alisema kuwa baada ya kupata elimu ya fedha amejua sehemu sahihi ya kutunza fedha zake kama vile benki, saccoss mbalimbali na vikundi vidogo vidogo vilivyosajiliwa.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa Serikali itahakikisha watu wote waliokusudiwa kupata elimu awamu ya kwanza wanafikiwa kama ilivyopangwa.
“Tumejipanga kutoa elimu kwa watu wote, watoa huduma na watumiaji huduma za fedha ili wawe na uelewa wa pamoja na mambo ya kuzingatiwa kuhusani wakati wa kutoa mikopo au kuchukua mikopo” alisema Bw. Kibakaya.
Kwa upande wake Afisa Biashara Mkoa wa Kagera na Mratibu wa Huduma za Fedha ngazi ya Mkoa, Bw. Keneth Mlilo, alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza kupata elimu ya fedha hususan kundi la kinamama kwa kuwa imeonekana kundi hilo ndilo waathirika wakubwa wa mikopo umiza yenye riba zisizolipika.
Mwisho