Tanzania imeikaribisha Jamhuri ya Korea ya Kusini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati na kilimo nchini Tanzania ili iweze kufikia lengo la kuwa na maendeleo endelevu.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Tanzania Jamhuri ya Korea Kusini Mheshimiwa Togolani Mavura, alipokuwa akitoa wasilisho kuhusu fursa zinazopatikana Tanzania wakati wa vikao vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Korea Kusini.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi yenye uchumi tulivu, amani na usalama na pia ina jiografia ya kimkakati ambapo nchi sita zinazopakana nayo zinategemea Tanzania kama mlango mkuu wa bahari.
‘‘Tanzania ina ardhi kubwa kufanikisha kilimo endelevu chenye kujali mazingira na ni nchi yenye vyanzo vingi vya kuweza kuzalisha umeme wa nishati jadidifu isiyochafua mazingira hasa ikizingatiwa kuwa dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi’’, alisema Mhe. Balozi Mavura.
Pia alisema kuwa Tanzania ina madini ya kimkakati ya graphite, nickel na lithium ambayo ndio madini yanayohitajika zaidi katika kuzalisha miundombinu na mitambo ya kuzalisha umeme wa nishati jadidifu.
Aidha, alizungumzia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu na bahari ambazo zinaweza kutumiwa na Korea kuja kuwekeza katika maeneo hayo ili kwa pamoja kuweza kufikia maendeleo endelevu.
Alifafanua kuwa kwa upande wa kilimo Tanzania inajielekeza katika maeneo manne ambayo ni uzalishaji wa ngano, mafuta ya kupikia, uzalishjaji wa matunda hasa parachichi, nyama na maziwa ambapo tayari Serikali imewekeza katika mradi wa mashamba makubwa kuwezesha vijana kulima kibiashara (BBT).
‘‘Tanzania ina fursa kubwa ya kuwa shamba la Afrika kuzalisha chakula kwa ajili ya Bara la Afrika ikiwa uwekezaji sahihi utafanyika katika kilimo cha kisasa,’’aliongeza Mhe. Balozi Mavura.
Nchi zilizotoa mawasilisho ni Tanzania, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Jamhuri ya Ivory Coast.