BENKI YA AfDB YAAHIDI DOLA BIL. 3.05 KUFADHILI MIRADI

Na. Saidina Msangi, WF, Busan, Korea Kusini.

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inatarajia kusaidia utekelezaji wa mradi wa
ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kipande cha Tabora
– Kigoma (lot 6) na Uvinza – Malagarasi (lot 7) kwa takribani dola za Marekani bilioni
3.05 na kufadhili maandalizi ya mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani
Zanzibar kwa takribani dola za Marekani milioni 60.

Hayo yameelezwa na Rais AfDB, Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina, alipokutana na
kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango –
Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya, pembezoni mwa vikao vya mkutano wa saba wa
Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC),
Mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini.

“Benki ya Mandeleo ya Afrika inafanyia kazi upatikanaji wa kiasi cha dola za
Marekani bilioni 3.05 kwa wakati ili kuwezesha kutekelezwa kwa mradi wa SGR kwa
manufaa ya Tanzania pamoja na nchi za jirani”, alieleza Dkt. Adesina.

Akizungumzia kuhusu ushirikishwaji wa Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi,
Dkt. Adesina alisema kuwa kuna umuhimu wa kuhusisha sekta hiyo katika
utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini Tanzania ili kuongeza kasi ya utekelezaji
wa miradi ya maendeleo na kukuza uchumi.

Dkt. Adesina alisisitiza kuwa ni vyema kuendeleza sekta binafsi kwa kuwa ni
muhimu katika kukuza uchumi kwa kasi na pia akaishauri Serikali kutumia fursa ya
dirisha la AfDB (non- Sovereign Window) kwa ajili yakuimarisha na kuwezesha sekta
binafsi nchini.

Aidha, alieleza kuwa Benki ya AfDB ipo tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kupiga
hatua kimaendeleo hasa katika miradi ya Kilimo, huku akiutaja mradi wa Kilimo wa
Building Better Tomorrow (BBT) kuwa utatoa ajira kwa vijana wengi na kuongezeka
kwa uzalishaji wa chakula nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango –
Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiongoza ujumbe wa Tanzania kwa niaba
ya Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), aliishukuru
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuongezea Tanzania mgao wa fedha
kupitia dirisha la mikopo nafuu (ADB) kwa mwaka 2023 kutoka UA 160 milioni sawa
na dola za Marekani milioni 216 hadi UA 560 milioni sawa na dola za Marekani
milioni 756.
 
Dkt. Mkuya alieleza kuwa kutokana na umuhimu wa miradi ambayo AfDB imeonesha
nia ya kuifadhili hususani mradi wa ujenzi wa bandari ya Mangapwani Zanzibar,
ameiomba Benki hiyo ione namna ya kuweza kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa
ajili ya kutekeleza mradi huo kabla ya mwaka 2025.
 
‘’Tayari tumefanya upembuzi yakinifu katika mradi wa bandariya Mwangapwani hivyo
upatikanaji wa fedha utawezesha mradi huo kuanza mara moja”, alieleza Dkt.
Mkuya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *