Benny Mwaipaja, Stockholm, Sweden
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), amewahakikishia wawekezaji katika nchi za Scandinavia ikiwemo Sweden kuwa Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kupitia upya masuala ya kodi na kifedha ili kuvutia uwekezaji zaidi wa mitaji kutoka nje ya Tanzania.
Dkt. Nchemba amesema hayo aliposhiriki mkutano wa wawekezaji, mjini Stockholm, Sweden, ulioitishwa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Grace Olotu, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Ubalozi huo kuimarisha masuala ya diplomasia ya kiuchumi.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania ni sehemu ya kimkakati ya kibiashara kutokana na ukubwa wa idadi ya watu waliopo katika eneo lote la Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na Ukanda wote wa Maziwa Makuu na kwamba Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuwataka wawekezaji hao wasaidie kuwahamasisha wawekezaji wengine zaidi kutoka nchi hizo za Scandinavia, kuwekeza nchini.
Alipigia chapuo maeneo muhimu ya uwekezaji yatakayokuza ajira na mauzo nje ya nchi kikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi, maeneo ambayo Serikali imewekeza fedha za kutosha lakini inahitajika mitaji na teknolojia itakayoongeza thamani ya mazao yatakayouzwa nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni. Pia alishawishi uongezaji thamani kwenye madini ndani ya nchi ikizingatiwa Tanzania ina madeni muhimu kama Nickel, Lithium na pia Graphite. Fursa kubwa kwenye kuanzisha viwanda vya madawa ya binadamu.
Aidha, aliieleza jumuiya hiyo ya wawekezaji kuwa hali ya uchumi wa Tanzania inaendelea kuimarika licha ya changamoto ya UVIKO 19, Vita baina ya Ukraine na Urusi, pamoja na kuyumba kwa soko la fedha za kigeni.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu, alisema mkutano huo na wawekezaji umelenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na nchi hiyo ulioanza tangu miaka ya 1930, na kwamba mkazo mkubwa hivi sasa ni kuimarisha zaidi diplomasia ya uchumi kwa kushawishi uwekezaji zaidi wa mitaji.
Kwa upande wao, baadhi ya wawekezaji hao ambao wamewekeza mitaji na tenolojia katika miradi mbalimbali wanayoitekeleza Tanzania Bara na Visiwani, wamepongeza hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hatua iliyowafanya wawekezaji wengine wengi kuendelea kutaka kuwekeza nchini Tanzania.
Dkt. Nchemba na ujumbe wake wako katika ziara ya kikazi nchini Sweden, ziara iliyolenga kuimaisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Sweden na Tanzania.