Na Eleuteri Mangi WUSM, Dar es Salaam
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameridhishwa na kasi ya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa utakaotumika kwenye ufunguzi wa Michuano ya African Football League (AFL) Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam.
Akiongea baada ya ya Waziri Dkt. Ndumbaro kumaliza kukagua maendeleo ya ukarabati wa uwanja huo Oktoba 02, 2023 jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema yapo mambo ambayo yanahitajika kukamilishwa kabla ya ufunguzi wa michuano hiyo ili kukidhi mahitaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kazi imefikia asilimia 70.
“Wengi mtakuwa mnakumbuka moja ya changamoto kubwa zilizopelekea hadi tukaanza kwenye heka heka kubwa kukarabati uwanja huu, ni changamoto ya taa. Hivi ninavyozungumza mkandarasi yupo anaendelea kufunga taa mpya, ndani ya siku mbili kazi hii itakuwa imekamilika, kwa hiyo kwa upande wa taa hatutakuwa na shida tutakamilisha ndani ya muda” Katibu Mkuu Bw. Msigwa.
Aidha, Katibu Mkuu Bw. Msigwa amesisitiza kuwa Waziri ametoa maelekezo kazi hiyo imalizike mapema zaidi ya muda uliopangwa ili Wakaguzi wa CAF watakapofika kati ya Oktoba 04 au 05, 2023 kwa ajili ya ukaguzi wa maendeleo ya Uwanja huo kabla ya ufunguzi wa mechi hiyo Oktoba 20, 2023.
Katibu Mkuu Bw. Msigwa ameongeza kuwa timu ya Wizara imepiga kambi katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa vile ili kuhakikisha hakuna kinachokwama.