Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili jijini New Delhi, India leo tarehe 08 Oktoba, 2023 kwa ajili ya kuanza ziara ya kitaifa ya siku nne nchini humo.
Mapokezi rasmi ya Mhe. Rais Dkt. Samia yatafanyika tarehe 09 Oktoba, 2023 ambapo atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa India, Mhe. Droupadi Murmu kwa pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Narendra Modi.
Ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini India ni mwendelezo wa ushirikiano na uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili ambapo sekta muhimu nchini kama Afya, teknolojia, kilimo, uchumi wa buluu, biashara, uwekezaji, maji na elimu zinatarajiwa kuwa kipaumbele cha majadiliano wakati wa ziara hii.