Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma ameipa mwezi mmoja Kampuni ya Beijing Construction Engeneering Group ikamilishe kazi zote zilizokua zimepangwa kutekelezwa mwezi Septemba zikamilike mwezi Novemba mwaka huu.
Mhe. Mwinjuma ametoa agizo hilo leo Oktoba 16, 2023 alipofanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa viwanja vya michezo na maeneo ya kupumzikia katika eneo changamani Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Mkandarasi huyo yupo nyuma ya muda wa utekekezaji wa mkataba kwa muda wa miezi miwili.
“Kazi hii inafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ilitakiwa imalizike mwezi Septemba. Nilikuja hapa Agosti 11, 2023 nikamuelekeza Mkandarasi aongeze kasi pamoja na nguvu kazi leo nimekuja naona bado kazi inasuasua ndio maana nimempa nafasi ya mwisho baada ya hapo hatutamvumilia” amesisitiz Mhe. Mwinjuma.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwinjuma amekagua Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya Ukarabati wa Awamu ya kwanza akiwaahidi Watanzania kuwa kazi hiyo itaendelea kwa Awamu ya pili kama ilivyopangwa.
Aidha, amewaalika Watanzania wafike uwanjani hapo kushuhudia mechi ya ufunguzi wa African Football League (AFL) kati ya timu ya Simba na Al Alhy ya Misri utakaochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Oktoba 20, 2023.