*Yawa ya Kwanza Barani Afrika kuwa Mwenyeji Mkutano wa Wakandarasi Waliowekeza kwenye Madini Chini ya Sakafu ya Bahari KUU*
Na Wizara ya Madini, Dar Es Salaam.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini kwa mara nyingine imeweka Historia ya kuwa Nchi ya Kwanza Barani Afrika kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Sita (6) wa Kimataifa wa Wakandarasi waliowekeza kwenye Madini yanayopatikana Chini ya Sakafu ya Bahari Kuu ambapo nchi inapata fursa ya kujifunza kuhusu utafiti, uvunaji na uendelezaji wa rasilimali hiyo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo wa Siku Tatu ulioanza leo tarehe Oktoba 22, 2023 jijini Dar es Salaam na utaendelea hadi Oktoba 24, 2023 huku ukitarajiwa kufungwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Kiruswa amesema umelenga kuwafahamisha washiriki kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maandalizi ya kuandaa Kanuni zitakazotoa mwongozo wa namna dunia itakavyonufaika na uvunaji wa rasilimali hiyo inayopatikana katika sakafu iliyo chini ya bahari kuu.
Ameongeza kwamba, pamoja na mambo mengine mkutano huo unatarajia kujadili ajenda mbalimbali kuhusu masuala ya utafiti, uchimbaji, utunzaji wa mazingira yaliyo chini ya sakafu ya bahari kuu ikiwa ni kuendelea na utekelezaji wa Article 145 ya UNCLOS Umoja wa Mataifa na makubaliano ya mwaka 1994 kuhusu shughuli za uchimbaji wa madini kwenye sakafu ya bahari.
‘’Nchi wanachama wa umoja wa Mataifa zinaandaa kanuni zitakazosimamia uvunaji wa rasilimali hizo kutokana na nchi nyingi duniani kuwa na wasiwasi kuhusu madhara ya kimazingira yanayoweza kusababishwa na shughuli za uchimbaji wa madini haya. ‘’ Kimsingi uchimbaji wa madini haya hauwezi kuharibu mazingira ya bahari bali madini haya yanachotwa kwa kutumia kifaa kiitwacho “collector” tu na kuletwa juu ya ardhi,’’ amefafanua Dkt. Kiruswa.
Akizungumza ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama wa umoja huo amesema ni nafasi kwa Tanzania kuendelea kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu rasilimali madini iliyo chini ya sakafu ya bahari ikiwemo kutafiti, kuvuna na kuiendeleza ili kunufaika ipasavyo na rasilimali hiyo ikiwa ni moja ya maeneo muhimu wa Uchumi wa Buluu.
Ameongeza kwamba, huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuendeleza rasilimali madini hususan madini muhimu na mkakati na kwa kuzingatia *Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri* ambayo inalenga kufanya utafiti wa kina kwa kutumia ndege angalau kufikia asilimia 50 ya eneo zima la nchi ifikapo mwaka 2030 ili hatimaye madini hayo yaweze kuongeza tija zaidi katika uchumi na mchango wa sekta ya Madini katika maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Madini yanayopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu (International Seabed Authority – ISA) Dkt. Marie Bourrel- MacKinnon ameipongeza Tanzania kuonesha dhamira ya uendelezaji wa madini hayo na kusema kwamba ushiriki wake katika mkutano huo utaisaidia kufanya maamuzi sahihi juu ya matarajio yake ya baadaye. Pia, ameongeza kuwa, mikutano kama hiyo inatoa fursa ya muhimu ya wanachama kujadili kwa kina na kutafakari namna bora zitakazowezesha kutoa uwiano sahihi na wa kutosha kwa maslahi ya wote.
Amesisitiza kuwa, wakandarasi hao wa madini yaliyo chini ya sakafu ya bahari kuu wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni zinazoongoza katika hatua mbalimbali za utafutaji wa madini hayo.
Awali, akizungumza katika ufunguzi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema Tanzania bado haina ujuzi na teknolojia za kutafiti na kuchimba madini yaliyochini ya sakafu ya bahari kuu hivyo, ushiriki wake na uwenyeji wake katika mkutano huo utaisaidia kujifunza, kupata ujuzi na kujengewa uelewa wa namna ya kuendeleza madini hayo.
Aidha, ameeleza kuwa, mkutano huo ni wa manufaa kwa Tanzania kwa kuwa utaiwezesha kujenga na kuimarisha mahusiano yatakayoisaidia kuendeleza rasilimali hiyo.
Kwa upande wa Tanzania, mbali na ushiriki wa viongozi na wataalam kutoka Wizara, Taasisi zake, pamoja na taasisi nyingine za umma, pia, umehudhuriwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Serikali kwenye Umoja wa Tanzania , Mhe. Balozi Hussein Kattanga.
Tanzania inashiriki ikiwa ni miongoni mwa nchi 169 wanachama wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Madini hayo (ISA) ambayo iko chini ya Umoja wa Mataifa yenye makao makuu yake Kingston nchini Jamaika.
Mkutano wa Sita umeshirikisha watu binafsi, na wawakilishi kutoka wakandarasi 15 huku wengine 16 wakishiriki kwa njia ya mtandao.
Mkutano huo hufanyika kila mwaka ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa shughuli zote za utafiti, uchimbaji na utunzaji wa mazingira yazingatiwa. Hadi kufikia sasa kuna wakandarasi wapatao 31 wa nchi zinazodhamini kutoka Ulaya, Amerika, Asia na Karibian ambazo zinaendela kutekeleza shughuli za utafiti wa madini aina ya Polymetalic Manganese Nodules (PMN), Sulphide na madini mengine yanayopatikana chini ya sakafu ya bahari ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa teknolojia za kisasa.
Aidha, mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu isemayo *Kuimarisha mahusiano na uwajibikaji katika usimamizi warasilimali za madini yaliyopo chini ya sakafu ya bahari kuu*