Kuanzia kesho, tarehe 30 Oktoba, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier, Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, atafanya ziara ya siku tatu nchini Tanzania kwa mwaliko wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nchi hizo mbili zinafurahia uhusiano bora na kufanya kazi pamoja katika sekta mbalimbali na maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Ziara hiyo italenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kwa kuzingatia biashara na uwekezaji. Rais Steinmeier atafuatana na ujumbe wa viongozi wa wafanyabiashara kutoka makampuni ya juu ya Ujerumani ambao watashiriki katika Jukwaa la Biashara na wenzao na viongozi wa Tanzania jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba.
Katika ziara hiyo, Rais Steinmeier atafanya mazungumzo rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam. Rais Steinmeier pia anatazamiwa kutembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji mjini Songea, na kuzungumza na vizazi vya wahanga wa vita hivyo.