Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier amewasili nchini leo tarehe 30 Oktoba 2023 kwa ziara ya kikazi ya siku tatu (3) kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi 1 Novemba 2023, na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Y. Makamba (Mb.) katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akiwa nchini Mheshimiwa Rais Steinmeier kesho Jumanne tarehe 31 Oktoba 2023 anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo watafanya mazungumzo na baadaye Viongozi hao wawili watapata fursa ya kuongea na waandishi wa habari kuelezea kuhusu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.
Katika Ziara hii ya Kikazi tofauti na Ziara ya Kitaifa Rais Steinmeier ambaye ameambatana ujumbe kutoka Serikalini na wafanyabiashara kutoka makampuni makubwa 12 ya nchini Ujerumani, kwa pamoja watashiriki katika ziara hiyio ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na biashara. Rais Steinmeier ataungana na mwenyeji wake Rais Samia kushiriki kwenye Jukwaa la Biashara kati ya Ujerumani na Tanzania litakalofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Mbali na kushiriki kwenye Jukwaa la Biashara Rais Steinmeier anatarajiwa kutembelea Kiwanda cha Twiga Cement jijini Dar es Salaam chenye ubia na Kampuni ya Scancem International ya Ujerumani kilichojengwa nchini mwaka 1967.
Ujerumani ni miongoni mwa Mataifa 10 duniani yanayongoza kwa uwekezaji nchini, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa miradi 178 kutoka nchini Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 408.11 imesajiliwa nchini kufikia mwezi Agosti 2023 ambayo imetengeneza ajira zipatazo 16,121.
Kwa upande wa Zanzibar miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300 imesajilia na kutengeneza ajira zipatazo 905.
Ujerumani na Tanzania zimekuwa katika uhusiano mzuri wa kidiplomasia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965, huku zikiendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo; maji, afya, matumizi endelevu ya rasilimali na utunzaji wa mazingira, uwezeshaji wa wanawake, usimamizi wa fedha, usawa wa kijinsia na michezo na utamaduni.