



Na. Josephine Majula, WF- Kagera
Wananchi wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwafikishia huduma ya elimu ya fedha itakayowakomboa kiuchumi na kuwaepusha na upotevu wa fedha.
Shukrani hizo zimetolewa na wananchi hao baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha iliyofanyika katika Ukumbi wa Kashura “Women Centre” uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata elimu hiyo, Bi. Ivona Gasper Mfanyabiashara alisema kuwa elimu aliyoipata ataenda kuwaelimsha wengine ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha.
“Tunaiomba Serikali iendelee kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wake na kuhakikisha inawafikia watu wote nchi nzima kwa sababu wananchi wengi wanapoteza fedha kwa kukosa elimu” alisema Bi. Gasper.
Mwelimishaji Rika Ngazi ya Jamii Bi. Jackline Petro, alisema kuwa baada ya kupata elimu ya fedha amejua sehemu sahihi ya kutunza fedha zake kama vile benki, saccoss mbalimbali na vikundi vidogo vidogo vilivyosajiliwa.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa Serikali itahakikisha watu wote waliokusudiwa kupata elimu awamu ya kwanza wanafikiwa kama ilivyopangwa.
“Tumejipanga kutoa elimu kwa watu wote, watoa huduma na watumiaji huduma za fedha ili wawe na uelewa wa pamoja na mambo ya kuzingatiwa kuhusani wakati wa kutoa mikopo au kuchukua mikopo” alisema Bw. Kibakaya.
Kwa upande wake Afisa Biashara Mkoa wa Kagera na Mratibu wa Huduma za Fedha ngazi ya Mkoa, Bw. Keneth Mlilo, alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza kupata elimu ya fedha hususan kundi la kinamama kwa kuwa imeonekana kundi hilo ndilo waathirika wakubwa wa mikopo umiza yenye riba zisizolipika.
Mwisho.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (katikati), akiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi (SCFEA) na mkutano wa Mashauriano ya Kibajeti wa Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Sudani Kusini, Mhe. Mhandisi Awow Daniel Chuang Deng, ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Baraza hilo, uliofanyika jijini Arusha, nchini Tanzania, ambapo Mawaziri hao wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo Wasilisho la nchi Wanachama kuhusu Miongozo ya Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 na Kaulimbiu za bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Ssemuwemba Mutaawe.
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden, Mhe. Diana Janse, jijini Dodoma, ambapo Naibu Waziri huyo, amemweleza Mhe. Dkt. Nchemba kuwa, nchi yake inaandaa Mkakati Mpya wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaolenga kuongeza ushirikiano katika Nyanja za kiuchumi na kibiashara.
Katika mazungumzo yao, Mhe. Dkt. Nchemba aliishukuru Sweden kwa kusaidia maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika sekta za nishati, elimu, maendeleo ya Jamii kupitia Mfuko wa TASAF pamoja na mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa SGR, kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida ambacho ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 96.
Aidha, Dkt. Nchemba ameishukuru Sweden kwa kuonesha nia ya kutoa zaidi ya dola za Marekani milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha reli ya kisasa SGR, fedha ambazo nchi hiyo itazitoa hivi karibuni baada ya kukamilika kwa tathimini ya mazingira ya mradi huo.
Kuhusu Mkakati Mpya wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Nchemba aliahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu katika kufanikisha mkakati huo na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Sweden kuja kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini ili kuchochea akuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Naibu Waziri huyo wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Diana Jense, alisema kuwa nchi yake inatambua kuwa mradi wa Reli ya Kisasa ni moja ya miradi ya kipaumbele kwa Tanzania na kwamba nchi yake iko tayari kushiriki katika ujenzi wa mradi huo.
Alisema pia kuwa mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Sweden utajielekeza zaidi katika masuala ya kiuchumi na kibiashara ambapo utalenga zaidi kuvutia uwekezaji kupitia sekta binafsi.
Aidha, katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Balozi wa Sweden Nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias na naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Chriastian Omolo, Viongozi hao walijadili kuhusu uwekezaji katika mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam ambapo nchi hiyo inataka kuwekeza kupitia kampuni ya Scania, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya usafiri katika jiji hilo la kibiashara.
Mwisho
Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WF, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, amesema Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), kupitia mpango uliotiwa saini mwaka 2014 limetoa ruzuku ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 139.5 sawa na Sh. bilioni 356.3 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Mwamba alibainisha hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea anayeshughulikia mambo ya kimkakati (KOICA) Don Ho Kim, aliye katika ziara ya kikazi Tanzania.
Alisema kuwa kupitia fedha hizo miradi kadhaa imekamilika na mingine inaendelea ambayo ni pamoja na Mfuko wa sekta ya Afya na Mpango Jumuishi wa Vijana Walio nje ya Shule (IPOSA).
‘‘Miradi kadhaa iko katika hatua mbalimbali za maandalizi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya usambazaji maji kwa maeneo ya mijini na vijijini mjini Dodoma na kuboresha usawa wa kijinsia katika Elimu (STEM) kwa Shule za Sekondari nchini ambapo miradi hii kwa sasa inapitia michakato ya kuidhinishwa ndani ya Wizara husika’’ alisema Dkt. Mwamba.
Alisema tangu 1991, KOICA imesaidia Serikali hasa katika nyanja za afya, elimu, maji na usafiri ili kubadilisha hali ya kijamii na kiuchumi nchini.
Dkt. Mwamba alisema kuwa kupitia mipango mbalimbali ya ufadhili, usaidizi wa kiufundi na programu za kujenga uwezo, KOICA imechochea mabadiliko chanya na yaliyosaidia ukuaji na ustawi jumuishi, kupambana na umaskini na kukuza uchumi.
Aidha alieleza kuwa Agosti 2023, Wizara ya Fedha iliwasilisha ombi la miradi minne ya maendeleo kwa msaada wa KOICA ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 39, sawa na Sh. bilioni 98, inayotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025.
Dkt. Mwamba alibainisha miradi hiyo kuwa ni mradi wa kuanzisha chuo cha ufundi Morogoro, mradi wa kuimarisha huduma za mama na mtoto jijini Dar es Salaam, mradi wa kuanzisha mifumo ya usambazaji maji katika maeneo ya vijijini vya mkoa wa pwani na mradi wa kuanzisha mpango kabambe wa kitaifa wa barabara kuu na uboreshaji wa uwezo wa rasilimali watu.
Dtk. Mwamba aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia KOICA kwa kuunga mkono malengo hayo ambapo imekuwa mojawapo ya vyanzo vikuu vya ufadhili wa ruzuku katika kufanikisha miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali zote zinazopatikana kutoka KOICA zinatumika kwa uangalifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ndani ya muda uliokubaliwa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) Don Ho Kim, alisema kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ya uchumi hasa katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, afya pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kuweza kunufaika na masoko.
Kuhusu miradi iliyowasilishwa na Tanzania alisema kuwa, ipo katika mchakato wa kuidhinishwa na Shirika hilo ambapo kati ya Novemba na Desemba mwaka huu inatazamiwa kuidhinishwa na Bunge la nchi hiyo, aliahidi nchi yake kuendeleza ushirikiano na kuunga mkono mipango ya maendeleo ya Tanzania
MWISHO.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) na Balozi wa Denmark hapa nchini, Mhe. Mette Dissing-Spandet (wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Fedha na Mkuu wa masuala ya Biashara-Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania, Bw. Oscar Mkude (wa nne kulia) baada ya kufanya mazungumzo yao, ambapo Dkt. Nchemba, ameishukuru nchi hiyo kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida. Mkutano huo umefanyika Katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha, Jijini Dodoma.