
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), akiwa na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. Ajay Banga, wametembelea mradi wa Kilimo cha Mwani katika kijiji cha Muungoni, Mkoanwa Kusini, Wilaya ya Kusini, Zanzibar, ambao umewezeshwa na Benki ya Dunia kupitia mfuko wa IDA, kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa mwani pamoja na kupanua wigo wa upatikanaji wa soko.

Bw. Banga, amezungumza na baadhi ya wanufaika wa mradi huo unaowanufaisha zaidi ya watu 15,000, ambapo asilimia 74 ni wanawake, na kuwahakikishia utayari wa Benki hiyo kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wakazi wa Zanzibar kupitia program mbalimbali wanazofadhili.

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza kuwa programu hiyo imesaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza uzalishaji wa mwani, pamoja na kupunguza gharama, na kuboresha maisha yao.
Ziara katika mradi huo ni mwendelezo wa matukio kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Tathmini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia (IDA20 Mid-Term Review) unaohusisha wakopaji, nchi Wahisani na Menejimenti ya Benki ya Dunia, ambao unafanyika katika Hoteli ya Golden Tulip (Airport)- Zanzibar, unaotarajiwa kuhitimishwa kesho tarehe 8 Desemba, 2023.

.