Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema mageuzi ya kidijitali Tanzania yamesaidia kufikiwa kwa huduma za kidijitali ikiwa ni pamoja na elimu na huduma za afya, kuboresha maisha ya watu, kuendesha soko shindani na ubunifu na kukuza ushirikishwaji.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan katika mdahalo wa mada isemayo: “Nchi yako iko tayari kujenga uchumi wa kidijitali?” katika jukwaa la Doha Forum lililowashirikisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Costa Rica Mhe. Arnoldo Andre Tinoco, Rais wa Mamlaka ya Mawasiliano Qatar Eng. Ahmad Almuslemani, Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa Taasisi ya Descartes Institute for the Future, Mkurugenzi wa Masoko Google Selim J.Edde, Mkuu wa Digitali (UNDP) Keyzom Ngodup ukiongozwa na Mwandishi wa kituo cha CNBC Dan Murphy katika ukumbi wa Hoteli ya Sheraton Doha, Qatar, tarehe: 11 Desemba 2023.
Aidha Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa dunia inabadilika katika suala la matumizi ya kidijitali na Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika hazipaswi kuachwa nyuma.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inatambua udhamira thabiti wa maono juu ya kuifikisha nchi kufikia malengo ya 4 ya dunia na Mapinduzi ya 5 ya viwanda yanayokuja.