TUNATAKA TTB ISONGE MBELE KATIKA UTANGAZAJI UTALI – WAZIRI KAIRUKI

Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kujipambanua ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo na kukua katika utangazaji utalii.

Ameyasema hayo leo Desemba 13,2023 jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Bodi ya Utalii Tanzania.

“Tunatamani tuache alama , nataka shirika hili liende mbele katika utangazaji utalii” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Ameitaka menejimenti ya bodi hiyo kujifanyia tathmini ili kujua ni kipi kinatakiwa kutekelezwa katika kutangaza utalii wa Tanzania hasa kupitia Wakurugenzi waliostaafu.

“Wasilianeni na Wakuu wa hii taasisi waliopita ili kujua zipi zilikuwa ndoto zao ambazo hawakuweza kuzifanikisha, na kipi kinafaa kuendelezwa na kuboreshwa ili kuinyanyua TTB” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Pia, ameitaka bodi hiyo kujenga utaratibu wa kuwasiliana na kushirikiana na balozi mbalimbali za Tanzania zilizopo nje ya nchi kwa kuwapatia taarifa muhimu za kutangaza utalii.

Kuhusu ustawi wa Watumishi Waziri Kairuki ameahidi kufanyia kazi changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha shirika hilo linafanya kazi ipasavyo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amewaasa Watumishi wa Bodi hiyo kuwa na utaratibu wa kujiendeleza kielimu ili kuendana na teknolojia hasa katika masuala ya utangazaji utalii.

Kuhusu mbinu za utangazaji utalii , Mhe. Kairuki ameitaka bodi hiyo kufanya tathmini juu ya mbinu mbalimbali za utangazaji utalii na pia kushirikisha wadau ili kujua bodi iko wapi na inaweza kufanya nini kuongeza idadi ya watalii nchini.

Tufanye uchunguzi wa aina mbalimbali za watalii tunaowahudumia kulingana na nchi wanazotoka, mahitaji yao, makundi maalum na kujua matumizi yao yakoje katika kutalii” amesema.

Aidha, amewataka watumishi wa TTB kushirikiana katika utendaji kazi kwa kuhakikisha Taasisi hiyo inakua na pia kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu hasa katika kukamilisha michakato yote ya kiserikali kama manunuzi, kusaini mikataba ya mashirikiano n.k.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Menejimenti ya TTB, baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya TTB pamoja na baadhi ya watumishi wa bodi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *