MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ZA ARDHI WACHANGIA ONGEZEKO LA WANAWAKE KUMILIKI ARDHI NCHINI

Mratibu Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Bw. Joseph
Shewiyo akifungua kikao kazi cha Asasi za kiraia kujadili utekelezaji wa mradi huo
Januari 16, 2024 jijini Dodoma.

Mtaalamu wa masuala ya Maendeleo ya Jamii kutoka Benki ya Dunia Bw. Nicholas
Soikan akisisitiza kuwa asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika Mradi wa
Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) na kuchangia kuinua uchumi wa mtu
binafsi, familia, jamii na taifa kwa ujumla ili kufikia malengo ya mradi huo.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na wahamasishaji kutoka asasi za kiraia kutoka
Chalinze, Shinyanga, Kahama, Nzega, Kigoma, Mufindi, Mbinga, Songwe, Tanganyika,
Maswa, Chamwino, Kaliua, Uyuwi, Nkasi, Chunya, Ludewa, Mkakete, Mvomero, Kilwa,
Ruangwa, Kilindi, Mkinga, Handeni, Ngara, Rorya, Iramba na Songea.

Na Eleuteri Mangi WANMM

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Serikali kwa
kushirikiana na Benki ya Dunia umeongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini
kutoka asilimia 25 hadi 35 hatua inayosaidia kuinua kiuchumi wao na taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mradi LTIP Bw. Joseph Shewiyo unaotekelezwa chini
ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati akifungua kikao kazi cha
Asasi za kiraia kujadili utekelezaji wa mradi huo Januari 16, 2024 jijini Dodoma.

“Mna jukumu kubwa, mnapaswa kuongeza wigo katika kutekeleza majukumu yenu
kufanikisha kutoa hati milki za kimila ili kuinua uchumi wa wananchi, mna mchango
mkubwa kwa ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 25 hadi 35,
mkafanye kazi yenu kwa weledi msiharibu ndoa za watu” amesema Bw. Shewiyo.

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia unalenga kuimarisha mifumo ya utawala
wa ardhi, kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wanaume na wanawake na hivyo
kukuza uwekezaji wa ardhi nchini.

Majukumu yanayotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuongeza usalama wa milki
za ardhi kwa kupanga, kupima na kumilikisha wananchi ardhi mijini na vijijini, kuboresha
mifumo ya usimamizi wa taarifa za ardhi nchini, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa
mradi.

Aidha, Asasi za Kiraia katika mradi huo zinajukumu la kutoa elimu kwa Jamii kuhusiana
na mradi, kutoa elimu kwa makundi maalumu kama vile wanawake, wazee, watoto na
watu wenye ulemavu kuhusu haki zao katika umiliki wa ardhi, kushiriki katika utatuzi wa
migogoro ya Ardhi, kutoa ushauri wa namna ya kushugulikiamasuala ya Jamii na
mazingira yanahusu mradi, kushirikiana na timu ya mradi katika kuandaa taarifa za
utekelezaji wa mradi hususani taarifa za masuala ya mazingira na jamii.

Kwa upande wake Mtaalamu Mkuu wa masuala ya Maendeleo ya Jamii kutoka Benki
ya Dunia Bw. Nicholas Soikan amesema kikao kazi hicho kina umuhimu mkubwa kwa

Uchumi wa mtu binafsi, familia, jamii na taifa kwa ujumla ili kufikia malengo ya mradi
huo.

Bw. Soikan ameongeza kuwa Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania
wanatambua umuhimu wa asasi za kiraia na zina nafasi ya kutatua migogoro ya ardhi
inayojitokeza wanapoishi ili kutekeleza mradi kwa ufanisi.

Kwa upande wao washiriki wa kikao kazi hicho kutoka asasi za kiraia Bw. Jesta
Twimanye kutoka Kahama na Bi Mwajumbe kutoka Mbinga wamesema kuwa
wamesema wanaendelea kushirikiana na Serikali katika mradi huo na wanaendelea
kutoa elimu juu ya haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake na wanaume na mradi
umesaidia kuongeza usalama wa ardhi kwa kutoa hati ya umiliki wa ardhi kwa mume na
mke.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na wahamasishaji kutoka asasi za kiraia kutoka
Chalinze, Shinyanga, Kahama, Nzega, Kigoma, Mufindi, Mbinga, Songwe, Tanganyika,
Maswa, Chamwino, Kaliua, Uyuwi, Nkasi, Chunya, Ludewa, Mkakete, Mvomero, Kilwa,
Ruangwa, Kilindi, Mkinga, Handeni, Ngara, Rorya, Iramba na Songea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *