Diplomasia ya Tanzania imezidi kung’ara kimataifa kufuatia viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali kufanya ziara nchini kwa lengo la kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), alipozungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam.
Akielezea ziara za viongozi hao nchini Waziri Makamba amesema tarehe 22 Januari 2024 atawasili Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Liu Guozhong ambaye atakuwa nchini tarehe 22 – 24 Januari , 2024.
“Mara baada ya kuwasili nchini, kiongozi huyo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko (Mb.),” alisema Waziri Makamba.
Amesema Kiongozi mwingine mkuu anayetarajiwa kuwasili nchini ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Mheshimiwa Salvador Valdes Mesa, ambaye atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 – 25 Januari, 2024. Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba.
Waziri Makamba, amesema Mheshimiwa Mesa anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson.
Pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere na kushiriki mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya Pan African Movement na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.
Kiongozi mwingine anayetarajiwa kuwasili nchini ni Rais wa Jamhuri ya Poland, Mheshimiwa Andrzej Duda atakayewasili nchini kwa ziara ya kikazi tarahe 8 – 9 Februari 2024.
Akiwa nchini, Mheshimiwa Duda atakutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Poland.
Amesema Tanzania na Poland zinashirikiana katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji, usimamizi wa mazingira, utalii, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa mabunge.
Aidha, ziara hiyo inatarajia kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama, nishati na gesi, madini, usafiri, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.
Mbali na viongozi wakuu wa mataifa tajwa kufanya ziara nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia tarehe 24 – 26 Januari 2024, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo. Ziara hiyo ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Agosti 2023.
“Ziara hii inalenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi,” aliongeza Waziri Makamba.
Kadhalika, Waziri Makamba amewaeleza waandishi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia pia kufanya Ziara ya Kitaifa Vatican tarehe 11 – 12 Februari, 2024 kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Francis.
Waziri Makamba ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Mhe. Pietro Parolin. Uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini. Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya. Kwenye ziara hiyo Mhe. Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo.
Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini Norway, tarehe 13-14 Februari 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja. Ameongeza kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwemo Mfalme Herald. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais pia atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na Kongamano la Nishati la Oslo,” alisema Waziri Makamba
Tanzania na Norway zinashirikiana kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.
Kuanzia mwaka 2010, Serikali ya Norway imekua ikishirikiana na Tanzania kwenye programu mbalimbali za maendeleo zilizo gharimu takribani TZS. 300 bilioni. Programu hizo zimesaidia na kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta ya Nishati; Sekta ya Elimu; Sekta ya Mafuta na Gesi; Mpango wa Usimamizi wa Fedha za Umma; programu za Mabadiliko ya Tabianchi; na programu za Usimamizi wa Misitu.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaandika historia kupitia ziara hii nchini humo kwani mara ya mwisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi hiyo kwa Ziara ya Kitaifa ilikua mwaka 1976.