Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) inaendelea kupanua wigo wa tafiti za wanyamapori kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii nchini ambapo, tarehe 13 Aprili 2024 zoezi la utiaji saini nyaraka za makabidhiano ya eneo la ujenzi wa kituo kipya cha utafiti Nyanda za Juu Kusini katika eneo Kihesa-Kilolo Mkoani Iringa kwa Mkandarasi limefanyika .
Ujenzi wa kituo hiko unatekelezwa kupitia mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) ambao umejikita kuboresha miundombinu, kuwezesha tafiti na kuboresha Maisha ya Jamii yanayozunguka hifadhi za Taifa za Udzungwa, Mikumi, Ruaha na Nyerere kwa utalii endelevu.
Akitia saini Nyaraka hizo kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Edward Kohi ambaye ni Mkurugenzi wa utafiti na mafunzo wa Wizara hiyo, amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya Utafiti itakayosaidia kupata taarifa za kisayansi zitakazo tumika kwa uhifadhi endelevu na kuandaa bidhaa za utalii kusini.
Aidha, Dkt.Kohi amesema kituo cha Utafiti Nyanda za Juu Kusini kina mchango mkubwa katika kukuza utalii ambapo amemtaka mkandarasi kufanya kazi ikiwezekana mchana na usiku ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo katika kipindi cha miezi 10 ya mkataba sambamba na TAWIRI kuhakikisha watumishi wa kituo hicho wanakuwepo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TAWIRI, Dkt Eblate Mjingo amebainisha manufaa ya kituo hicho ni kuharakisha zoezi la kufanya, kusimamia na kuratibu Tafiti za wanyamapori katika eneo la kusini pamoja na kuwezesha ukaribu baina ya wadau wa uhifadhi, watafiti na waongoza utalii waliopo maeneo ya kusini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi TAWIRI, Dkt.David Manyanza amesema Kituo cha Nyanda za Juu Kusini kitawezesha juhudi za Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan za kuitangaza nchi kupitia vivutio vyake ikizingatiwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa Maliasili ya Wanyamapori katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la kusini.
TAWIRI ina vituo vinne vya utafiti ambavyo ni Njiro – Arusha, Serengeti , Kingupira, Kituo cha Magharibi na Kituo hiki kipya cha Nyanda za Juu Kusini kinakamilusha idadi ya vituo vitano.