MIAKA MIWILI YA FILAMU YA TANZANIA THE ROYAL TOUR, MABALOZI WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA ONGEZEKO LA WATALII.

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro Kreta.

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Ujerumani, Ufaransa na Ubelgiji wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kutangaza utalii wa Tanzania zilizopelekea kuendelea kuongeza idadi ya watalii hapa nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na mabalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Tanzania Nchini Ujerumani Hassan Idd Mwamweta na Balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa Mhe. Ali Jabir Mwadini walitotembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuona vivutio vya utalii, uboreshaji wa huduma na kushuhudia idadi kubwa ya wageni wa nchi wanazowakilisha wakifurahia vivutio vya nchi yetu.

Kiongozi wa mabalozi hao Mhe. Jestas Nyamanga ameeleza kuwa nchi ya Ubelgiji pekee ina takribani watalii 16,000 wanaotembelea nchi ya Tanzania kila mwaka na kwamba juhudi zinaendelea kufaywa na ofisi ya ubalozi kuendelea kuongeza idadi hiyo.

“Kwa sasa ni takribani miaka miwili tangu uzinduzi wa filamu ya Royal tour uliofanywa na Mhe. Rais, filamu hii imeitangaza nchi yetu hasa katika bara la ulaya tulipo na imeongeza uelewa wa vivutio tulivyonavyo, Nchi ya ubelgiji pekee ina zaidi ya watalii 16,000 wanaotembelea Tanzania na tumeweka mikakati ya kuongeza mara dufu” ameongeza Mhe. Nyamanga.

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Hassan Mwamweta ambaye pia anasimamia nchi za Poland, Switzerland, Vatican, Hungary, Romania, Bulgaria na jamhuri ya Czech ameleeza kuwa mahusiano mazuri ya diplomasia ya Uchumi yaliyofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nchi hizo yamesaidia viiongozi wa nchi hizo kutembelea Tanzania na kuendelea kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na utajiri wa vivutio vya utalii tulivyonanvyo.

Akiwa katika bonde la Ngorongoro balozi wa Tanzania Nchini Ufaransa Mhe. Ali Mwadini amekutana na watalii kutoka Ufaransa ambao wamemueleza kuwa Wameijua zaidi Tanzania kupitia filamu ya Royal tour iliyofanywa na Mhe, Rais na kushawishika kutembelea Tanzania kwa muda wa siku 8 Zanzibar na Ngorongoro na wameahidi kuwa mabalozi wazuri watakaporudi nchini kwao.

Katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro pekee kati ya Julai 2023 hadi mwezi machi, 2024 Jumla ya watalii 750,220 ambapo watalii wa ndani ni 283,460 na watalii wa nje 466,760 wametembelea hifadhi ya Ngorongoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *