MAELEKEZO YA RAIS SAMIA YATEKELEZWA, KONGAMANO LA UWEKEZAJI SEKTA YA UTALII LAFUNGULIWA RASMI

Na Mwandishi Wetu- Arusha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe.Prof. Kitila Mkumbo leo Aprili 30, 2024 amefungua rasmi Kongamano la Uwekezaji kwenye Sekta ya Utalii katika Mkoa wa Arusha lenye kauli mbiu isemayo “Uwekezaji katika Utalii Endelevu: Changamkia Fursa za Uwekezaji Baada ya Programu ya Tanzania-The Royal Tour”.

Kongamano hilo lenye lengo la kuboresha Sekta ya Utalii ni maelekezo mahususi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo aliagiza Wizara ya Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili kukaa kwa pamoja na kuja na mikakati ya uwekezaji itakayoboresha sekta hiyo mkoani Arusha.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa ni muhimu Sekta Binafsi na Serikali kushirikiana katika kuhakikisha kuna miundombinu bora katika maeneo ya hifadhi pamoja na huduma za malazi zilizoboreshwa ili kuvutia watalii wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, amewahakikishia wadau wa utalii kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuitangaza nchi kimataifa, itaendelea kuboresha miundombinu katika maeneo yenye vivutio vya utalii na kuboresha huduma katika mnyororo wa thamani wa shughuli za utalii na pia kuainisha vivutio maalum kwa ajili ya uwekezaji kwenye Sekta ya Utalii.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb),Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu Maliasili, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Mbaga Kida, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mhe. Paul Makonda, Viongozi Waandamizi wa Chama na Serikali pamoja na Wadau wa Uhifadhi na Utalii wa jijini Arusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *