Na. Jacob Kasiri – Mbarali.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewahakikishia wananchi wa Mbarali na Watanzania kwa ujumla kuwa zoezi la kuwarejesha wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo litakuwa ni endelevu na lenye kuleta tija na ufanisi kwa wananchi wanaokaa kandokando mwa Hifadhi ya Taifa Ruaha na Pori la Akiba Mpanga-Kipengele.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 09.05.2024 Wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya alipokwenda kuzindua na kushiriki zoezi la kufukuza Tembo katika Kata tano za Igava, Mawindi, Miyombweni, Imalilosongwe na Rujewa ambazo ndio waathirika wakubwa wa kadhia hiyo.
Akiwa katika zoezi hilo aliwahakikishia wananchi hao na watanzania kwa ujumla kuwa , “Zoezi hili si la muda mfupi, ni matumaini yangu litaleta tija na ufanisi mkubwa kwa wananchi wetu, najua changamoto mliyokuwa nayo ndio maana Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kulishughulikia kwa haraka. Ndani ya muda mfupi mtaona mabadiliko makubwa.”
Aidha, Mhe. Kairuki aliongeza kuwa kwa siku mbili wataalam wetu wamefanikiwa kuwaswaga na kuwarudisha hifadhini takribani tembo 61, huku jana makundi matano yenye tembo 43 na leo tembo 18 wamerejeshwa katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Ili kupunguza vifo visivyo vya lazima, Mhe. Kairuki alisema, “Tembo wanapovamia maeneo yenu msijichukulie sheria mkononi kwa kuwauwa, kwa kawaida tembo huwa ana tabia ya kulipiza kisasi, lazima mtambue kuwa hata ikipita miaka mingi tembo hasahau eneo alilouwawa mwenzao au alipopata kadhia na bughuza, akipita eneo hili na akakutana na binadamu lazima alete taharuki na kujueruhi.”
Mbali na kuwarejesha tembo hao hifadhini, zoezi hilo linaenda sambamba na ufungwaji wa mikanda maalum ya mawasiliano kwa tembo kiongozi kwenye kila kundi. Kwa namna mikanda hiyo ilivyo kisasa pindi watakavyosogea karibu na maeneo ya watu, mikanda hiyo yenye vifaa vya kielektroniki itatuma taarifa ya uwepo wao kwa wahifadhi ambao watafika mara moja kabla hawajavuka maeneo yaliyohifadhiwa na hivyo kusaidia jamiii kuondokana na changamoto za uharibifu wa mali.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mbarali Mhe. Bahati Ndingo (Mb) aliishukuru Wizara na taasisi zake akisema, “Niwapongeze wataalam kutoka TANAPA, TAWA, TAWIRI na TFS kwa kufanya kazi usiku na mchana, matokeo yameonekana, hivyo wana Igava, Ikanutwa na maeneo mengine ambapo zoezi hili linafanyika tutapata ahueni .”
Zoezi la kuwaondoa tembo hao katika mashamba ya wananchi na kuwarejesha hifadhini lilianza jana tarehe 08.05.2024 na linaendelea ambapo mpaka leo jioni tembo takribani 61 wamerejeshwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.